• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 PM
WANTO WARUI: KNEC itafakari tena kuhusu hatua ya kutotahini insha chini ya mtaala wa CBC

WANTO WARUI: KNEC itafakari tena kuhusu hatua ya kutotahini insha chini ya mtaala wa CBC

NA WANTO WARUI

KATIKA ratiba ya mtihani wa mwisho wa Gredi ya 6 (KPSEA) iliyotolewa na Baraza la Mitihani nchini Nchini (KNEC), masomo mawili muhimu, insha ya Kiswahili na ile ya Kiingereza hayakuwepo miongoni mwa masomo yatakayotahiniwa.

Kukosekana kwa masomo haya huenda kutaathiri mfumo mzima wa CBC kwa kuwa masomo hayo ni muhimu mno katika maisha ya wanafunzi.

Ikiwa masomo haya hayatatahiniwa na KNEC, hivyo ni kusema hayana maana kufunzwa. Walimu hawatakuwa wakiyafunza shuleni kwa vile watayapuuza licha ya kuwa yanafaa kufunzwa.

Vile vile, wanafunzi wenyewe hawatakuwa wakiyatilia maanani kabisa. Kutokana na hilo, kutakuwa na kasoro kubwa sana katika ufunzaji hata wa masomo mengine kwa kuwa uandishi ndio nguzo ya masomo mengine.

Kutowafunza wanafunzi kuandika ni kosa kubwa na njia kuu ya kuua vipawa vya uandishi miongoni mwa wanafunzi.

Ikiwa wanafunzi hawatafunzwa uandishi, basi taifa litapata wapi waandishi wa vitabu, magazeti, majarida na mambo mengine mengi yanayohitaji uandishi wenye ubunifu? Ni vipi kutakuwepo wasomi bila uandishi? Kazi nyingi sana katika taifa hutegemea maandishi, na maandishi hayo huwa yamefunzwa shuleni. Mojawapo ya kazi ambazo hutegemea sana masomo ya insha na lugha ni kazi za mahakimu na mawakili. Hatuwezi kuwa na mawakili au majaji ambao hawajui kuandika. Watafanya kazi zao namna gani?

Makarani kortini watatayarisha maandishi na barua muhimu namna gani?

Ni vipi mawasiliano yatawezekana bila uandishi? Masomo ya uandishi ndiyo msingi wa elimu. Ndiyo huwezesha wanafunzi kuelewa masomo mengine pia. Masomo mengine husomwa kutokana na msingi uliowekwa kupitia masomo ya lugha. Bila lugha, hakuna mawasiliano na hivyo elimu.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Malalamishi ya wagombeaji yasipuuzwe na...

Uhasama wa Kihika, wabunge tishio kwa kura za Ruto Nakuru

T L