• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
KNH kuzika miili 541 wenyewe wasipoenda kuichukua

KNH kuzika miili 541 wenyewe wasipoenda kuichukua

Na HILARY KIMUYU

HOSPITALI ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) inapanga kuzika maiti za watu 541 zilizoko kwenye hifadhi ikiwa jamaa zao hawatazitambua ndani ya siku saba zijazo.

Miongoni mwa maiti hizo ni za watoto 475 na watu wazima 66 ambao huenda wakazikwa katika kaburi la halaiki ikiwa familia zao hazitawatambua katika siku za hivi karibuni.

Kulingana na taarifa kutoka hospitali hiyo, saba kati ya miili ya watu wazima ni wa jinsia ya kike huku wengine 59 waliosalia wakiwa wanaume.

“Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta ina maiti kadhaa katika hifadhi yake ambazo hazijadaiwa na familia zao,” hospitali hiyo ikasema katika notisi kwa umma.

Katika notisi hiyo iliyotolewa wiki hii katika chapisho la MyGov, KNH ilisema hatua inayopanga kuchukua inaambatana na hitaji la Sheria ya Afya ya Umma Sura ya 242 ya 1991 na Kanuni ya Mochari za Umma.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Afya ya Umma Sura ya 242, umma unaombwa kutambua na kuchukua maiti hizo ndani ya siku saba la sivyo hospitali itasaka kibali kutoka kwa mahakama kuzizika katika kaburi la halaiki,” KNH ikasema.

Kulingana na orodha iliyotolea na KNH, watoto ndio hutelekezwa zaidi baada ya kufa na hivyo maiti zao kurundikana katika hifadhi ya maiti ya hospitali hiyo. Idadi kubwa ya watoto hufa wakitibiwa katika hospitali na familia na jamaa zao hukosa kudai maiti zao.

Sheria ya Afya ya Umma inahitaji kwamba maiti ambayo haitadaiwa iondolewe kutoka mochari ndani ya wiki mbili.

Isipoondolewa, maiti hiyo inapasa kuzikwa katika kaburi la halaiki baada ya maafisa wa umma kupata kibali kutoka kwa mahakama.

KNH ilisema orodha ya majina ya watu ambao maiti zao hazijachukuliwa imewekwa katika ubao wa matangaza katika hifadhi yake ya maiti. Aidha, majina hayo yanaweza kupatikana katika tovuti ya hospitali hiyo ya rufaa.

Hospitali kadhaa katika Kaunti ya Nairobi zimeendelea kubeba mzigo wa kuhifadhi maiti zisizodaiwa katika mochari zao. Wiki jana, serikali ya Kaunti ya Nairobi ilitoa makataa ya siku saba kwa wakazi kutambua na kuchukua maiti za wapendwa wao katika mochari za City, Hospitali ya Mama Lucy Kibaki na Hospitali ya Mbagathi.

Endapo maiti hizo 185 hazitachukuliwa kabla ya kukamilika kwa muda huo, serikali ya Kaunti ya Nairobi itazizika kwenye kaburi la halaiki.

Mochari ya City inahifadhi maiti 130 ambazo hazijadaiwa, Hospitali Mbagathi ina maiti 838 huku ile ya Mama Lucy Kibaki ikiwa na maiti 17 ambazo jamaa zao hawajadai.

Maiti hizo zililetwa katika mochari hizo kati ya Septemba 2021 na Desemba 2023 na maafisa wa polisi.

  • Tags

You can share this post!

Gachagua amtembelea hospitalini polisi aliyedungwa mishale...

Iko wapi gesi ya Sh500? Kilio mtungi wa kilo 13 ukiongezeka...

T L