• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:55 PM
KOMBE LA DUNIA 2022: Jacob ‘Ghost’ Mulee apongeza juhudi za makocha Waafrika

KOMBE LA DUNIA 2022: Jacob ‘Ghost’ Mulee apongeza juhudi za makocha Waafrika

NA RUTH AREGE

KOCHA wa zamani wa Harambee Stars Jacob ‘Ghost’ Mulee anasema, wakufunzi wandani wanafaa kupewa nafasi ya kunoa timu za taifa. 

Kwa mara ya kwanza, timu za Afrika katika Kombe la Dunia zitasimamiwa na makocha wa ndani ambao ni wachezaji wote wa zamani wa timu ya taifa.

Aliou Cisse, kiongozi wa mabingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika, Senegal, anawaongoza makocha wengine wanne kutinga hatua hiyo kubwa zaidi ya soka.

Makocha wengine wa Afrika wanaopeleka mataifa yao katika Kombe la Dunia ni Jalel Kadri (Tunisia), Walid Regragui (Morocco), Rigobert Song (Cameroon) na Otto Addo (Ghana).

Mulee amesisitiza kuwa, kuwaajiri makocha wa kigeni kunoa timu za taifa ni fikra za kikoloni ambazo  Afrika imekuwa nazo kwa muda mrefu na zinafaa kupigwa teke na kuondoka Afrika.

“Nina furaha sana na ninajivunia makocha wenzangu wa Kiafrika kushughulikia timu tano kwenye Kombe la Dunia. Ni kihistoria na mwanzo wa safari ndefu kuelekea mabadiliko ya fikra kutoka kwa serikali na mashirikisho,” Mulee alisema.

Mulee alikuwa kocha wa mwisho mzaliwa wa Kenya kuipeleka Harambee Stars katika michuano ya Mataifa Bingwa Afrika (AFCON) mwaka wa 2004.

Mwenzake Francis Kimanzi anasema, haijalishi kocha anatoka wapi kuongoza timu ya taifa katika jukwaa kubwa kama kombe la dunia.

“Kocha ni kocha tu haijalishi anatoka wapi, masomo ya ukocha yanafanana dunia nzima. Kocha anaweza kuwa mzuri lakini ikiwa wachezaji sio wazuri, hawawezi kumsaidia kujenga folosofia yake,” alisema Kimanzi.

Naamini makocha wa Afrika katika michuano ya Kombe la Dunia, nina imani watawashangaza wengi kombe la dunia,” aliongezea Kimanzi.

Kimanzi anasema ataungana nyuma ya wababe wa Afrika Senegal. Senegal, kwa sababu ya uthabiti wao katika mashindano ya AFCON na Kombe la Dunia na Uholanzi kwa sababu ya falsafa na mtindo wao wa uchezaji.

Mtaalamu huyo alikuwa sehemu ya benchi ya ufundi ya aliyekuwa kocha mkuu wa Stars Sebastien Migne katika AFCON ya mwaka 2019 nchini Misri akiwa na Harambee Stars.

You can share this post!

Waiguru hatarini kupoteza nyumba

Majeraha yalemaza Ufaransa huku Benzema akiungana na Kante,...

T L