• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
KPA imeajiri Wapwani kupita kiasi, yadai ripoti

KPA imeajiri Wapwani kupita kiasi, yadai ripoti

Na MWANDISHI WETU

MAMLAKA ya Bandari za Kenya (KPA) huenda ikalazimika kutengea jamii zenye asili ya nje ya Pwani nafasi zaidi za ajira kuliko Wapwani.

Kamati ya Seneti inayosimamia masuala ya utangamano wa kitaifa, imetoa agizo hilo baada ya kubainika idadi ya waajiriwa katika bandari ambao ni Wapwani imezidi idadi inayokubaliwa kisheria.

Hali hii katika KPA sio tofauti katika mashirika mengine ya umma nchini, kwani imekuwa kawaida jamii za eneo yalipo kuwa na wafanyikazi zaidi kuliko wa kutoka maeneo mengine.

Kwa mujibu wa ripoti iliyowasilishwa katika Seneti, waajiriwa kutoka jamii za Wamijikenda ni 2,274 kati ya watu 6,470 walioajiriwa KPA kijumla.

Wamijikenda wanajumuisha makabila ya Wadigo, Wachonyi, Wakambe, Waduruma, Wakauma, Waribe, Warabai, Wajibana na Wagiriama na wengi wao wanapatikana katika Kaunti za Kilifi na Kwale.

Idadi ya Wataita ambao pia ni mojawapo ya jamii za asili ya Pwani ni 496.

Hata hivyo, ripoti hiyo inaonyesha kuwa nafasi nyingi za ngazi za juu katika KPA zinashikiliwa na watu wanaotoka katika jamii ambazo si za asili ya Pwani.

Hawa wanajumuisha waajiriwa 10 kutoka kwa jamii ya Waluo, wakifuatwa na tisa kutoka jamii ya Wakikuyu.

Kwa jumla, kuna nafasi 23 kubwa za kiusimamizi katika shirika hilo la kiserikali.Kulingana na Sheria ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa iliyopitishwa mwaka wa 2008, ni marufuku kwa jamii moja kushikilia zaidi ya theluthi moja ya nafasi za kazi katika shirika lolote la kiserikali.

“KPA inafaa ianze mara moja kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa kunapotokea nafasi mpya za ajira zitajazwa kwa misingi ya Kikatiba na sheria nyingine zifaazo kuhusu hitaji la kuwa na makabila tofauti ili kuzipa nafasi jamii nyingine,” kamati hiyo ilisema.

Ripoti hiyo sasa imetilia shaka madai ya viongozi wa Pwani kuhusu ubaguzi dhidi ya jamii za eneo hilo kiajira katika KPA ambayo husimamia bandari ya Mombasa.

Ripoti hiyo imetokea wakati KPA inatarajiwa kuanzisha mchakato wa kuajiri watu zaidi ya 900 ambao watachukua nafasi za wale wanaotarajiwa kustaafu kufikia mwaka wa 2023.

“KPA haikuonyesha thibitisho la hatua ambazo zimepangwa kuchukuliwa kuhakikisha nafasi mpya zitajazwa kwa msingi wa Katiba na sheria nyingine zifaazo,” kamati ya seneti ikaeleza.

Kwa miaka mingi, suala la ajira bandarini limekuwa likiibua malalamishi mengi kutoka kwa viongozi wa Pwani ambao hutaka nafasi za usimamizi zitengewe Wapwani ili vijana wengi eneo hilo waajiriwe.

Mnamo Julai 2021, uamuzi wa Mahakama ya Ajira iliyo Mombasa ndio ulifanikisha kuajiriwa kwa Bw John Mwangemi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa KPA baada ya mivutano iliyodumu kwa muda mrefu.

Bw Mwangemi alichukua nafasi ya Bw Rashid Salim ambaye alistaafu.

Bw Salim alikuwa ameshikilia nafasi hiyo kama kaimu kwa zaidi ya mwaka mmoja baada ya Bw Daniel Manduku kujiuzulu ghafla Machi 28, 2020 alipohusishwa na sakata ya ufisadi.

You can share this post!

Kenya yakabiliwa na kibarua kigumu dhidi ya Misri kutafuta...

TAHARIRI: Serikali itoe ARVs bora kwa watoto ili kuzuia vifo

T L