• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:50 AM
LAPSSET: Kampuni za uchukuzi wa meli zafurika Lamu kutafuta fursa za kibiashara

LAPSSET: Kampuni za uchukuzi wa meli zafurika Lamu kutafuta fursa za kibiashara

Na KALUME KAZUNGU

KAMPUNI 10 za usafiri wa meli zinazoongoza ulimwenguni ni miongoni mwa 40 ambazo tayari zimezuru Bandari Mpya ya Lamu (LAPSSET) wakati ambapo kiegesho cha kwanza cha mizigo bandarini humo kinatarajiwa kufunguliwa rasmi mwezi huu wa Oktoba.

Mapema Agosti 2019, Bodi inayoshughulikia Ujenzi na Maendeleo ya LAPSSET (LCDA) ilitangaza kukamilika kwa kiegesho hicho cha kwanza huku viegesho vingine viwili vya kwanza vikitarajiwa kukamilika kufikia Desemba 2020.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Afisa Mkuu Mtendaji wa LAPSSET, Bw Silvestre Kasuku, amesema Alhamisi kwamba wameshuhudia kampuni nyingi za meli ambazo hivi karibuni zimekuwa zikizuru bandari ya Lamu ili kutafuta mwanya na fursa za kibiashara na uwekezaji pindi LAPSSET itakapoanza kutekeleza shughuli zake rasmi.

Inatarajiwa kwamba baadaye Oktoba, kiegesho hicho cha kwanza kitafunguliwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Miongoni mwa kampuni tajika za usafiri wa meli ulimwenguni ambazo zimezuru bandari ya Lamu ni pamoja na Maersk kutoka Denmark, Evergreen Marine Corp, Mediterranean Shipping Company (MSC), Pacific International Line (PIL), Ocean Network Express (ONE), Hapag Lloyd, CMA CGM Group, China Ocean Shipping (Group) Company-COSCO na Hyundai Merchant Marine (HMM).

Afisa Mkuu Mtendaji wa LAPSSET, Bw Silvestre Kasuku (kulia) awahutubia wawakilishi wa kampuni maarufu za usafiri wa meli baharini. Picha/ Kalume Kazungu

Bw Kasuku amesema juma hili pekee wamepokea wawakilishi wa zaidi ya kampuni 20 za meli ambao walifika kujionea bandari ya Lamu katika harakati za kuitangaza bandari hiyo kibiashara ulimwenguni.

“Wiki hii pekee tumepokea zaidi ya wawakilishi wa kampuni za meli 20 kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu, ikiwemo bara Uropa, Amerika, Afrika na hata Asia. Wote walikuja kuzuru bandari ya Lamu wakati huu ambapo matayarisho ya ufunguzi wa kiegesho cha kwanza yanaendelea. Kufikia sasa, zaidi ya kampuni 40 za uchukuzi wa meli zimefika hapa kujionea kinachoendelea na kutafuta fursa ziliopo kibiashara hasa tangu kiegesho cha kwanza kukamilika,” akasema Bw Kasuku.

Alifafanua kwamba kila aliyefika alifurahishwa na maendeleo ya LAPSSET na kuishukuru serikali ya Kenya kwa kuibuka na mradi kama huo

“Tunatarajia biashara itanoga zaidi pindi shughuli za bandari ya Lamu zitakapoanza rasmi,” akasema.

Bandari hiyo inatazamiwa kufungua eneo la Lamu na Kaskazini mwa Kenya kwa jumla hasa kibiashara na kiviwanda.

Bandari ya Lamu pia inatarajiwa kuimarisha uhusiano wa kibiashara hasa miongoni mwa mataifa ya Afrika Mashariki, Mashariki ya Kati na ulimwengu mzima kwa jumla.

Bandari ya Lamu itahudumia soko la nchi ya Ethiopia ambayo kwa sasa hutegemea bandari ya Djibouti na ile ya Sudan Kusini katika shughuli zake za uchukuzi wa mizigo.

Bandari ya Lamu inajumuisha viegesho 32 wakati itakapokuwa imekamilika.

  • Tags

You can share this post!

Sakaja aelezea kutoridhishwa kwake na kuteuliwa kwa Mary...

Seneti yazimwa kumjadili Samboja

adminleo