• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
Luis Suarez afunga goli lake la 500 kitaaluma na kudumisha Atletico kileleni mwa jedwali la La Liga

Luis Suarez afunga goli lake la 500 kitaaluma na kudumisha Atletico kileleni mwa jedwali la La Liga

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI mahiri raia wa Uruguay, Luis Suarez, 34, alifunga bao lake la 500 katika taaluma ya kusakata soka ya kitaaluma mnamo Jumapili usiku na kusaidia waajiri wake Atletico Madrid kuchapa Alaves 1-0 kwenye Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Bao hilo la pekee na la ushindi kwa Atletico lilifumwa wavuni na Suarez baada ya kupokezwa krosi safi na beki Kieran Trippier katika dakika ya 54.

Goli hilo lilikuwa la 19 kwa Suarez kupachika wavuni tangu aanze kuvalia jezi za Atletico ya kocha Diego Simeone mwanzoni mwa msimu huu wa 2020-21. Awali, sogora huyo anayejivunia mabao 63 kutokana na mechi ambazo amechezea Uruguay, alikuwa amefungia Barcelona mabao 198 na kupachikia Liverpool jumla ya magoli 82.

Kipa Jan Oblak aliokoa penalti iliyochanjwa na Joselu mwishoni mwa kipindi cha pili na kuhakikisha kwamva Atletico wanasalia kileleni mwa jedwali la La Liga kwa alama 66, nne zaidi kuliko nambari mbili Barcelona waliopepeta Real Sociedad 6-1.

Suarez alianza taaluma yake ya kusakata soka akivalia jezi za Club Nacional nchini Uruguay ambapo alifunga mabao 12 kabla ya kujiunga na kikosi cha Groningen cha Ligi Kuu ya Uholanzi (Eredivisie) alikopachika wavuni jumla ya magoli 15.

Aliingia baadaye katika sajili rasmi ya Ajax nchini Uholanzi mnamo 2007 na akafunga mabao 111 kabla ya kusajiliwa na Liverpool mnamo 2011 kisha Barcelona mnamo 2014.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ingwe Youth wapania kuoanda ngazi msimu huu

Re Union yapiga moyo konde kujikaza kupanda ngazi