• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Mabadiliko ya Tabianchi: Afrika pia sharti iwajibike

Mabadiliko ya Tabianchi: Afrika pia sharti iwajibike

NA PAULINE ONGAJI

KONGAMANO la 2022 la Umoja wa Mataifa kuhusiana na mabadiliko ya tabianchi, al-maarufu COP 27 lilizinduliwa rasmi Jumapili katika eneo la Sharm El Sheikh, nchini Misri.

Katika kongamano hili ambalo ni la 27 na linalotarajiwa kuendelea kati ya Novemba 6 na 18, mataifa ya bara la Afrika yanatarajiwa kupaza sauti kuhusu ajenda waliyonayo, hasa ikizingatiwa kwamba hafla hii inaandaliwa barani.

Mojawapo ya masuala yanayotarajiwa kujadiliwa kwa kina ni ufadhili kutoka mataifa yaliyostawi ili kugharimia majanga yanayolikumba bara hili kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, nchi za Afrika zinatarajiwa kushinikiza mataifa yaliyostawi kupunguza uzalishaji wa gesi ambazo zimethibitishwa kuongeza kiwango cha halijoto ardhini (greenhouse gasses), na hivyo kuchangia pakubwa mabadiliko ya tabianchi.

Utafiti wa kisayansi umeonyesha kwamba mataifa yaliyostawi ndio yamechangia pakubwa uzalishaji wa gesi hizi ikiwa ni pamoja na dioksidi ya kaboni kupitia ustawi wao.

Uchunguzi zaidi umeonyesha pia hata kipimo cha uzalishaji wa gesi hizi kwa kila mtu katika mataifa haya ni zaidi kikilinganishwa na mataifa maskini.

Kwa upande mwingine, licha ya kuwakilisha chini ya asilimia 4 pekee ya uzalishaji wa gesi hizi hatari, Afrika inaendelea kuathirika pakubwa na janga hili huku wataalamu wakitabiri ongezeko la halijoto barani ikilinganishwa na sehemu nyingine zozote ulimwenguni.

“Lakini, inapowadia wakati wa kubeba mzigo, mataifa maskini, Afrika ikiwemo, yameendelea kuumia. Kwa mataifa yaliyostawi, huenda mabadiliko ya tabianchi yanaathiri kiwango cha joto au baridi, lakini kwa Afrika, athari hizi zinatugusa katika maisha yetu ya kila siku kama vile ukosefu wa mvua, maji, ukame, chakula na hatimaye umaskini,” aeleza Dkt Paul Matiku, mwanaekolojia na mtaalamu wa uhifadhi na ustawi wa rasilimali, vile vile mkurugenzi mtendaji katika shirika la uhifadhi mazingira la Nature Kenya.

Miezi michache iliyopita, jopo kuhusu mabadiliko ya tabianchi linalohusisha serikali kadhaa IPCC, lilizindua utafiti ulionyesha kwamba katika kipindi cha miaka saba iliyopita, viwango vya joto ulimwenguni vilikuwa vya juu zaidi kuwahi shuhudiwa, huku Afrika ikiathirika pakubwa.

Mifugo ikiwa imeangamia kutokana na kiangazi kikali. PICHA | MAKTABA

Katika eneo la Afrika Mashariki wanasayansi wametoa onyo kwamba athari za ongezeko la halijoto tayari zimeanza kushuhudiwa. Hapa nchini, The State of the Climate – Kenya 2020 Report iliyotolewa na Idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini, inaonyesha kwamba viwango vya joto vilivyorekodiwa mwaka wa 2020 vilikuwa vya juu vikilinganishwa na kipindi kati ya 1981 na 2012.

Mabadiliko haya, kulingana na wataalamu, yanatarajiwa kusababisha vipindi vya ukame na njaa hasa katika maeneo ya Afrika mashariki na kuathiri pakubwa sekta ya kilimo. Na tayari athari hizo zimeanza kushuhudiwa.

Baadhi ya sehemu za bara hili zinakumbwa na vipindi vya ukame huku sehemu zingine zikiathirika na mvua na mafuriko na hivyo kusababisha vifo na hasara. Aidha mataifa ya Afrika Kusini yamekumbwa na vipindi vya mafuriko and dhoruba.

Hapa nchini, kwa mujibu wa tafiti kadhaa kuhusu hali ya anga, mzunguko wa vipindi vya ukame umekuwa mfupi kiasi kwamba sasa unashuhudiwa kwa wingi.

Wanawake wakipakua magunia ya mtama kutoka kwa lori la Shirika la Chakula Duniani (WFP) mjini Gumuruk, Sudan Kusini. Ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN) ya Novemba 3, 2022 inasema watu 8 milioni nchini Sudan Kusini wanakabiliwa na njaa. PICHA | AFP

Kwa sasa zaidi ya watu milioni 52 katika upembe wa Afrika wanakabiliwa na njaa kufuatia ukame mbaya zaidi kuwahi shuhudiwa katika kipindi cha miaka 40. M kufuatia ukame mbaya zaidi kuwahi shuhudiwa katika kipindi cha miaka 40.iongoni mwa mataifa haya ikiwemo Sudan, Somalia, Kenya, Ethiopia na eneo la Karamoja nchini Uganda.

Nchini Kenya, hali ya hatari imetangazwa katika zaidi ya kaunti 23 huku zaidi ya watu milioni 3.5 wakikabiliwa na njaa.

Ndiposa wataalamu wanasisitiza wakati umefika kwa mataifa yaliyostawi kuwajibika na kuanza kugharimia majanga ambayo yametokana na ustawi wao.

“Mbali na kushinikiza mataifa yaliyostawi kuhakikisha upungufu wa uzalishaji wa gesi hizi hatari, Afrika inapaswa kupaza sauti ili kuhakikisha kwamba ahadi za ufadhili zilizotolewa na mataifa haya matajiri zimetimizwa bila masharti,” aeleza Dkt Matiku.

Mataifa yanayostawi yamekuwa yakishinikiza mataifa matajiri kuhakikisha kwamba ufadhili wa hasara inayotokana na majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, unafikia angaa dola 100 bilioni kila mwaka kufikia mwaka wa 2020.

Lakini huku mataifa ya Afrika yakiendelea kushinikiza nchi zilizostawi kuwajibika katika masuala haya ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi, pia serikali za hapa barani haziepuki lawama.

Wataalamu wanasema kwamba kwa kiwango fulani, shughuli za uharibifu wa mazingira nyumbani pia zimechangia pakubwa. Kwa mfano ukataji haramu wa miti, mbinu duni za kilimo, na uvamizi wa ardhi iliyotengewa misitu kunachangia hali inayoshuhudiwa.

Kulingana na anuwai iliyotolewa mwaka jana, kwa sasa Kenya haijafikisha asilimia 10 ya misitu ambayo ni kiwango cha chini zaidi kinachohitajika kimataifa, kwani ni asilimia ya 7.2 pekee yenye misitu.

Hali hii imesababisha ukame na uhaba wa mvua na maji. Hapa nchini tayari chemichemi tano kuu za maji – Mlima Kenya, Aberdare Range, Mau Complex, Cherangani Hills na Mlima Elgon, ambazo zinatoa takriban asilimia 75 ya rasilimali za maji – zimeripotiwa kupunguka.

“Athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimeanza kujitokeza na kuathiri kiwango cha maji zimetokana na mabadiliko ya matumizi ya ardhi,” aeleza to John Mwangi, mwanasayansi wa matumizi ya rasilimali za ardhi na maji katika Taasisi ya mafunzo ya Centre for Training and Research in ASAL Development.

Kulingana na Dkt Matiku, hata ingawa ni sharti mataifa yaliyoendelea yawajibikie suala hili,serikali za mataifa yanayostawi na hasa hapa barani Afrika pia zinapaswa kubeba mzigo huu.

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Kwa kuvipuuza vyuo vikuu Kenya Kwanza...

Wazazi wa ndugu wawili waliouawa Kianjakoma watoa ushahidi...

T L