• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Madagascar tayari kwa mtihani wa Tunisia katika 8-bora

Madagascar tayari kwa mtihani wa Tunisia katika 8-bora

Na MASHIRIKA

ALEXANDRIA, MISRI

LICHA ya ulimbukeni wao katika kampeni za AFCON, Madagascar wanapigiwa upatu kuendeleza ubabe wao katika kivumbi hicho watakapovaana leo Alhamisi saa nne usiku na Tunisia katika robo-fainali uwanjani Al Salam, Misri.

Sawa na Tunisia waliowabandua Ghana kwenye hatua ya 16-bora, Madagascar nao walijikatia tiketi ya robo-fainali kupitia mikwaju ya penalti ambapo walizamisha DR Congo.

Baada ya kuwaduwaza miamba kadhaa wa soka ya Afrika, Madagascar ambao wameyapiku matarajio ya mashabiki wengi, kwa sasa si kikosi cha kupuuzwa tena nchini Misri.

 

Fowadi harles Andriamahitsinoro (kulia) wa Madagascar akabiliwa na kiungo wa DR Congo, Jacques Maghoma (kushoto) Julai 7, 2019, uwanjani Alexandria, Misri. Picha/ AFP

Hii ikiwa mara yao ya kwanza kuwania ubingwa wa taji la AFCON, Madagascar almaarufu Barea walikamilisha kampeni zao za Kundi B kileleni baada ya kusajili sare ya 2-2 dhidi ya Guinea kisha kuwakomoa Burundi 1-0 na kuwazima Nigeria kwa mabao 2-0.

Ni ufanisi uliowapa tiketi ya kuvaana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika hatua ya mwondoano.

Sare 2-2

Wakitegemea pakubwa huduma za kiungo Anicet Andrianantenaina na fowadi Charles Andriamahitsinoro, Madagascar ambao wanaorodheshwa wa 108 duniani, walizidi maarifa DR Congo kupitia mikwaju ya penalti baada ya kuambulia sare ya 2-2 mwishoni mwa muda wa ziada.

Isipokuwa Andrianantenaina, kocha Nicolas Dupuis ambaye ni mzawa wa Ufaransa, amepania kutegemea zaidi maarifa ya wachezaji wanaowajibikia vikosi vya madaraja ya chini nchini Madagascar.

Kwa upande wao, Tunisia walikamilisha kampeni zao za Kundi E katika nafasi ya pili baada ya kuambulia sare tatu dhidi ya Angola, Mali na Mauritania.

  • Tags

You can share this post!

Kinda ghali zaidi duniani atua Atletico

SIHA NA LISHE: Epuka vyakula hivi mara kwa mara kwa ajili...

adminleo