• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:12 PM
Madaraka Dei 2021: Miaka 58 ya uhuru, Wakenya wana yapi ya kujivunia?

Madaraka Dei 2021: Miaka 58 ya uhuru, Wakenya wana yapi ya kujivunia?

Na SAMMY WAWERU

HUKU Rais Uhuru Kenyatta leo Jumanne akiongoza taifa kuadhimisha miaka 58 ya uhuru wa Kenya kuna masuala kadha wa kadha yanayopaswa kuwekwa kwenye mizani.

Juni 1, 1963, Kenya ilipata uhuru wa kujitawala kutoka kwa Waingereza, siku ambayo huadhimishwa kila mwaka nchini.

Mzee Jomo Kenyatta (babake rais wa sasa Uhuru Kenyatta), aliongoza kukomboa nchi kutoka kwa minyororo ya wakoloni dhalimu.

Miaka 58 baadaye, ni yapi, hasa miradi ya maendeleo yameafikiwa?

Umaskini ungali kero kuu kwa Wakenya wengi.

Kufuatiaia takwimu za hivi punde za shirika la utafiti la Afrobarometer, kiwango cha umaskini (Kenya’s Lived Poverty Index – LPI) kimepanda kutoka 0.93 hadi 1.06, kati ya 2014 na 2018.

Ripoti ya shirika hilo inaeleza, nusu ya idadi jumla ya Wakenya wanakosa mahitaji muhimu ya kimsingi kama vile maji safi, chakula na dawa.

Afrobarometer inasema asilimia 47 ya Wakenya hawawezi kumudu chakula mara tatu kwa siku, hasa baada ya janga la Covid-19 kutua nchini 2020, huku asilimia 55 wakilalamikia kushindwa kumudu gharama ya matibabu.

Zaidi ya Wakenya milioni 7.8 wanaishi katika kiwango cha umaskini uliokithiri.

Kulingana na Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS), kwenye ripoti yake mnamo 2020, zaidi ya vijana milioni tano nchini wenye uwezo kufanya kazi hawana ajira, jambo ambalo linazidisha gapu kati ya tajiri na maskini.

Kwa mujibu wa KNBS, kiwango cha ukosefu wa kazi 2020 kilipanda mara dufu hadi asilimia 10.4 kikilinganishwa na asilimia 5.2 mwaka 2019.

Takwimu za KNBS pia zinasema Wakenya 1,716,604 walipoteza kazi kati ya Aprili na Juni 2020.

Idadi ya walioajiriwa imeshuka hadi Wakenya milioni 15.9 kutoka milioni 17.8.

Sekta ya afya

Huduma za afya zinaendelea kuimarika. Kulingana na takwimu za Wizara ya Afya (MoH), 2001 Kenya ilikuwa na vituo 4,421, kufikia sasa idadi ikipanda hadi 10,466.

Wizara ya Afya inakiri ukosefu wa fedha za kutosha kuboresha huduma za afya ungali kikwazo.

Licha ya huduma za afya kuboreka, ghrama ya matibabu inaendelea kupanda.

Kulingana na wizara, asilimia 11 pekee ya idadi jumla ya Wakenya wana bima ya afya ya NHIF, inayomilikiwa na serikali.

Huku zaidi ya asilimia 70 ya Wakenya wakiwa katika sekta ya juakali na biashara ndogondogo na za kadri, wengi wao hawana uwezo kumudu bima ya kibinafsi.

Afya bora na nafuu kwa wote ni moja ya Ajenda Nne Kuu za Rais Uhuru Kenyatta, lakini miaka minne baadaye, hilo halijafanikiwa.

Maendeleo

Huku uchumi ukitajwa kukua kwa asilimia 5.4 mwaka 2019, sekta ya kilimo, misitu na samaki ilishuka kutoka asilimia 6.0 hadi 3.6.

Sekta ya viwanda ilikua kwa asilimia 3.2, kutoka asilimia 4.3 mwaka 2018.

Kimsingi, miundomsingi kama vile barabara na nguvu za umeme, inaendelea kuimarika.

Mashambani hata hivyo, serikali ina kibarua kutokana na ubovu wa baadhi ya barabara zinazotatiza shughuli za usafiri na uchukuzi msimu wa mvua.

Maji na chakula

Kwa mujibu wa UNICEF, asilimia 59 pekee ya Wakenya wanapata maji. Nchini, watu milioni 9.9 wanakunywa maji ambayo hayajatibiwa.

Kulingana na taasisi ya Kenya Institute for Public Policy Research Analysis, Wakenya milioni 14.5 hukumbwa na janga la njaa kila mwaka, hasa wanaoishi maeneo kame.

  • Tags

You can share this post!

Fowadi wa zamani wa Brighton na Palace, Glenn Murray,...

Pwani wasema hawana cha kusherehekea Madaraka Dei