• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Madiwani 15 wa Nyandarua kujibu madai ya kujitengea mamilioni

Madiwani 15 wa Nyandarua kujibu madai ya kujitengea mamilioni

Na WAIKWA MAINA

TUME ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) imeagiza madiwani 15 wa Kaunti ya Nyandarua kujibu madai ya kujitengea Sh3.6 milioni kinyume cha sheria katika mwaka huu wa kifedha.

Mkuu wa EACC eneo la Kati, Bw Charles Rasugu, alisema madiwani hao wanatarajiwa kufika mbele ya wachunguzi Jumanne, Jumatano na Alhamisi huku baadhi ya madiwani maalum, wakitarajiwa kuitwa baadaye kuhojiwa kuhusiana na madai hayo.

Hata hivyo, madiwani hao walihusisha hatua hiyo na siasa wakisema ni wale wanaompinga Spika Wahome Ndegwa walioitwa kufika mbele ya maafisa wa EACC.

Diwani wa wadi ya Shamata, Bw Gitau Njamba alisema kwamba hawajapokea barua yoyote kutoka kwa EACC na kwamba wako tayari kujiwasilisha wakiitwa rasmi.

“Tumeona nakala ya barua ya EACC inayotaja majina yetu ikisambazwa katika mitandao ya kijamii. Hatuelewi ni kwa nini nakala ilisambazwa katika mitandao ya kijamii kabla ya kuwasiliana nasi rasmi. Tunaona siasa katika suala hili nzima lakini tuko tayari kufika mbele ya EACC mawasiliano rasmi yakifanywa. Hatuna sababu ya kuwa na wasiwasi, kuogopa na hatuna chochote cha kuficha,” alisema Bw Gitau.

Alilalamika kuwa nakala inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii haielezi wanacholaumiwa kuhusiana nacho kuwawezesha kujiandaa kuandikisha taarifa.

Bw Rasugu anasema kila diwani aliyeitwa alipokea Sh240,000 za kukarabati ofisi lakini hakuna kazi waliyofanya.

“Hayo ni madai tu ambayo tunalenga kuchunguza, na ndio sababu tumewaita kuandikisha taarifa nasi, kufika kwao kutatupatia mwelekeo tutakaofuata uchunguzi ukikamilika,” alisema Bw Rasugu.

Alipuuza madai kwamba EACC imeingiza siasa na kuungana na Spika Wahome akisema ni jukumu la tume kuchunguza madai yote yanayohusiana na ufisadi.

“Malalamishi ni kwamba madiwani hao walipokea pesa katika akaunti zao binafsi ambazo hawakufaa kupata. Hii ilikuwa wakati kulikuwa na mzozo wa uongozi katika bunge la kaunti, kama wako hawana kosa, EACC haitakuwa na shida nao,” aliongeza Bw Rasugu.

You can share this post!

Obado aanza kusaka ufuasi eneo la Pwani

Kasisi Dolan ataka jamii zisaidie kulinda haki za binadamu

T L