• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 10:50 AM
Magharibi, Pwani na Mashariki kuamua mrithi wa Rais Uhuru

Magharibi, Pwani na Mashariki kuamua mrithi wa Rais Uhuru

NA LEONARD ONYANGO

MAENEO ya Magharibi, Mashariki na Pwani yataamua mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta baada ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Ripoti ya utafiti wa kura ya maoni uliofadhiliwa na kampuni ya Nation Media Group inaonyesha kuwa maeneo hayo yana idadi kubwa ya watu ambao hawajaamua ikiwa watampigia kura Naibu wa Rais William Ruto au kinara wa Azimio la Umoja One-Kenya, Bw Raila Odinga.

Kulingana na utafiti huo uliofanywa na Infotrak wikendi iliyopita, Bw Odinga anaungwa mkono na asilimia 55 ya wakazi wa Pwani huku Dkt Ruto akifuatia kwa asilimia 29.

Lakini asilimia 13 ya wakazi wa eneo hilo hawajamua.

Iwapo Dkt Ruto atafanikiwa kuvutia kundi hilo la wakazi wa Pwani ambao hawajaamua, atamkaribia Bw Odinga ambaye amekuwa na ushawishi mkubwa katika eneo hilo kwa muda mrefu.

Dkt Ruto anaungwa na magavana wawili wa Pwani; Salim Mvurya (Kwale) na Amason Kingi wa Kilifi ambaye aligura muungano wa Azimio wiki iliyopita na kujiunga na Kenya Kwanza ambapo ameahidiwa kuwa spika wa Seneti.

Bw Odinga atahitaji kuimarisha kampeni zake katika maeneo ya Kwale na Kilifi ili kuzuia Dkt Ruto kuvuna wafuasi zaidi.

Utafiti huo pia unaonyesha kuwa Dkt Ruto na Bw Odinga wako nguvu sawa katika eneo la Mashariki ambapo kila mmoja ana asilimia 40.Eneo la Mashariki linajumuisha Kaunti za Kitui, Machakos, Makueni, Marsabit, Meru, Tharaka Nithi, Embu na Isiolo.

Iwapo kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka atatulia ndani ya Azimio endapo atakosa kuteuliwa kuwa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga, idadi ya kura za waziri mkuu huyo wa zamani huenda ikaongezeka.

Lakini Bw Musyoka akijiondoa Azimio au akiunga mkono Dkt Ruto, kura za Bw Odinga katika eneo la Mashariki zitapungua kwa kiasi kikubwa hivyo kuwa baraka kwa Naibu wa Rais.

Asilimia 14 ya wakazi wa eneo la Mashariki hawajaamua ikiwa watamchagua Dkt Ruto au Bw Odinga.

Japo Bw Odinga anaongoza kwa umaarufu katika eneo la Magharibi kwa asilimia 48 huku Dkt Ruto akifuatia kwa asilimia 33, bado ana kibarua kigumu kuhakikisha kuwa anaongeza ushawishi wake eneo hilo.

Iwapo asilimia 12 ya wakazi wa Magharibi ambao hawajaamua wataegemea upande wa Naibu wa Rais, Bw Odinga atajipata pabaya.Bw Mudavadi na Seneta wa Bungoma wameahidi kumpa Dkt Ruto asilimia 70 ya kura za Magharibi ili kuwawezesha kupata mgao wao wa asilimia 30 ya viti serikalini.

Hiyo ina maana kuwa wawili hao huenda wakakita kambi katika eneo hilo ili kutimiza ahadi yao kwa Naibu wa Rais.

Kaunti ambazo huenda zikaegemea upande wa Dkt Ruto ni Bungoma na Vihiga ambazo ni ngome za Bw Wetang’ula na Bw Mudavadi mtawalia.

Asilimia 11 ya wakazi wa Kaskazini Mashariki ambao hawajaamua ndio watakaotoa mwelekeo ikiwa Dkt Ruto au Bw Odinga ndiye atazoa kura nyingi katika eneo hilo.

Utafiti wa Infotrak unaonyesha kuwa Bw Odinga anaongoza kwa asilimia 48 huku Dkt Ruto akifuatia kwa asilimia 37.

Kaunti nyingine zenye ushindani mkubwa ambazo zinatazamwa kama zilizo na uwezo wa kuamua rais wa tano wa Kenya ni Kajiado, Narok, Turkana, Samburu, Trans Nzoia na Nairobi.

  • Tags

You can share this post!

Chelsea, Liverpool ni kisasi tu fainali ya FA

Mkataba wa Musalia, Ruto watatiza Mlima

T L