• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
Magongo: Vikings yafanya kulihali kurejea katika mashindano ya Ligi Kuu

Magongo: Vikings yafanya kulihali kurejea katika mashindano ya Ligi Kuu

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya wanawake ya Vikings ni kati ya vikosi saba vinavyoshiriki mechi za mpira wa magongo ya Supa Ligi kuwania tiketi ya kufuzu kurejea kucheza Ligi Kuu muhula ujao.

Warembo hawa chini ya kocha, Clyde Mbaha wanapitia hali ngumu kifedha ambayo imechangia kutofanya vizuri baada ya kushushwa ngazi msimu uliyopita.

”Katika mpango mzima tunasaka wadhamini ili kutupiga jeki maana tumepania kurejesha ubora wa mchezo wetu,” alisema mwanzilishi na meneja wake, Marie Aran na kuongeza kuwa wanatamani sana kuwa kati ya klabu mahiri nchini katika mchezo huo kama miaka iliyopita.

Meneja huyo anasema imekuwa vigumu kwa wachezaji wa kikosi hicho kufanya mazoezi ya pamoja ili kuzoeana vizuri na kujiweka sambamba tayari kukabili wapinzani wengine kwenye kampeni za kipue hicho.

”Timu yetu inajumuisha wachezaji ambao ni wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka maeneo tofauti nchini ikiwamo Kisumu, Nairobi, Meru, Machakos na Bungoma,” akasema.

Anadokeza kuwa baada ya Bank of Afrika kukatiza ufadhili wao wamejikuta njia panda maana hawawezi kugharamia nauli ya wachezaji kila wiki angalau siku moja kuhudhuria mazoezi ya pamoja.

Anashikilia kuwa bila marafiki kuwachangia hela imekuwa vigumu kusafiri kushiriki mechi za ligi za maeneo ya mbali kama Mombasa. Hata hivyo inabahatika kwa kuzingatia timu nyingine tano zipo Nairobi.

Miaka iliyopita Vikings ilikuwa kati ya vikosi vilivyokuwa vinatetemesha katika mchezo huo nchini kwenye kampeni za Ligi Kuu.

Timu hiyo ilikuwa inatikisa wapinzani wengine wakiwamo malkia wa mchezo huo Blazers awali wakifahamika kama Telkom Orange.

Kocha anasema ana kikosi cha chipukizi ambao endapo watapata ufadhili watapata motisha zaidi pia kujituma kutoa ushindani mkali dhidi ya wapinzani wao.

”Bila kujipigia debe endapo nyakati zingine hutumia hela zetu binafsi kugharimia nauli ili kushiriki mechi za ligi tukipata wadhamini tutafanya kinyume na matarajio ya wengi,” nahodha wake, Grace Obima alisema na kutoa kilio kwa wafadhili wajitokeze kuwapiga jeki ili kuwapa nafasi kukuza talanta zao.

Awali timu ya Vikings ilikuwa moto wa kuotea mbali katika Ligi Kuu ya Hoki au Magongo. PICHA | JOHN KIMWERE

Vikings imekuwa ikishiriki kampeni za Ligi Kuu tangia mwaka 2000 hadi msimu uliopita ilipoteleza na kulazimika kuteremshwa ngazi.

Kwenye kampeni za Ligi Kuu inajivunia wakati moja ilipobahatika kumaliza katika nafasi tatu bora.

Ingawa inashiriki ngarambe ya kiwango cha chini mwanzilishi huyo anasema, wanatamani kupiga mechi za Ligi Kuu na kufuzu kushiriki kipute cha Klabu Bingwa Afrika (AFCON) miaka ijayo.

Katika jedwali, Vikings inavuta mkia katika nafasi ya saba kwa alama moja baada ya kushiriki mechi nne. Nao wasomi Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) wamo kileleni kwa kusajili alama 10, tano mbele UoN Ladies pia JKUAT Ladies na MMU.

  • Tags

You can share this post!

DCI yamsaka mshukiwa mkuu wa mauaji ya Samuel Mugoh Muvota

Voliboli: Wawakilishi wa Kenya wawasili nchini Tunisia...

T L