• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Maimamu waapa kujiunga na maandamano ya kupinga SGR

Maimamu waapa kujiunga na maandamano ya kupinga SGR

Na Mishi Gongo

MAIMAMU kutoka misikiti ya Mombasa wameapa kujiunga na madereva wa matrela na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu katika maandamano ya kila Jumatatu katika mji huo, kupinga amri ya serikali kusafirisha mizigo kupitia treni ya SGR.

Maimamu hao waliokongamana jana katika ukumbi wa Ujamaa Mombasa, walisema hawatasitisha maandamano hayo hadi pale serikali itakapobadilisha amri hiyo.

Kongamano hilo lillilohudhuriwa na maimamu kutoka Shanzu, Changamwe, Likoni, Kisauni, na Mvita pamoja na wanachama wa shirika la Fast Action Movement na Haki Africa.

Imam Rashid Oricho kutoka msikiti wa Mwinyikombo Jomvu, aliiomba serikali kuweka mikakati itakayohakikisha kuwa uchumi wa Mombasa unaimarika.

Alisema tangu kutolewa kwa amri ya usafirishaji mizigo kutumia SGR, wakazi wengi katika mji huo wamepoteza kazi zao.

Mwenzake, Abdulhakim Katana kutoka msikiti wa Zabibu Shanzu, alisema si madereva wa matrela walioathirika na ujio wa SGR bali wapwani wote kwa jumla.

Walisema wanahofia kuongezeka kwa ujambazi kufuatia vijana wengi kupoteza kazi zao.

Imam Shehe Juhudi kutoka msikiti Noir Changamwe alisema japo serikali ilileta ugatuzi kunufaisha watu mashinani, Wapwani hawajanufaika na chochote.

Mwenyekiti wa First action Movement Bw Salim Karama alisema hawaungi mkono mpango wa maridhiano BBI wakiutaja mpango huo kama mbinu ya viongozi kujinyakulia mali.

Afisa wa maswala ya dharura katika shirika la Haki Africa, Mathias Shipeta alisema maandamano hayo yatajumuisha washikadau mbali mbali kuhakikisha kuwa serikali inaangazia suala hilo.

You can share this post!

Kanisa la ACK kupokea sadaka kwa M-Pesa kuzima ufisadi

Msichana ‘aliyefufuka’ avutia umati

adminleo