• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 2:37 PM
Majengo kadhaa sasa kubomolewa kupisha Jiji Eldoret

Majengo kadhaa sasa kubomolewa kupisha Jiji Eldoret

TITUS OMINDE NA BARNABAS BII

MAJENGO kadhaa ya biashara mjini Eldoret yameratibiwa kubomolewa baada ya serikali ya Kaunti kuweka masharti magumu kwa wamiliki wa mali katika kampeni ya kurembesha na kupandisha hadhi ya jiji.

Kulingana na idara ya mipango ya kaunti hiyo, takriban majengo 10 haramu ya thamani ya mamilioni ya pesa yamelengwa kubomolewa chini ya sheria mpya.

Majengo yanayolengwa ni pamoja na yale yaliyojengwa kwenye njia za kupitishia maji-taka au kwenye ardhi ya umma huku mengine yakiwa na kasoro na kuhatarisha naisha ya wapangaji na wakazi wa mji.

“Baadhi ya majengo haya yako kwenye ardhi ya umma au njia za mifereji ya maji huku mengine yakiwa na kasoro na yanapaswa kubomolewa,” meneja wa Manispaa ya Eldoret, Bw Julius Kitur akasema.

Wamiliki wa majengo waliopewa notisi wameanza kubomoa majengo hayo huku wengine wakisimamisha kazi za ujenzi.

Hata hivyo, baadhi ya wawekezaji wamekabiliana na mchakato wa ubomoaji wakisema kuwa utawatisha wafadhili na kuumiza uchumi wa taifa.

“Kaunti inahitaji kubuni mikakati inayofaa kuwashawishi wawekezaji ikizingatiwa kuwa wengi wao wamehamia mikoa mingine au kupunguza biashara kutokana na matatizo ya kiuchumi,” mmoja wa wawekezaji, Bw Hassan Kosgei akaambia Taifa Leo.

Kadhalika, alisema baadhi ya majengo ya zamani yaliyotengwa kwa ajili ya ubomoaji yanapaswa kukarabatiwa huku mji huo ukitazamiwa kupandishwa hadhi kuwa jiji.

Miongoni mwa mambo makuu ya kuzingatiwa ni pamoja na kuwajibika kwa wamiliki wa majengo kupaka rangi majengo yenye rangi inayofanana isiyohusishwa na chapa yoyote ya kibiashara au kukabiliwa kwa kutozwa faini au kifungo cha miezi sita jela na kutwaa tena ardhi ambayo haitumiwi.

Kulingana na Meneja wa Manispaa ya Eldoret, Bw Tito Koiyet wawekezaji wanatakiwa kutii sharia jipya la sivyo wachukuliwe hatua kali.

“Wawekezaji wote lazima wazingatie sheria zinazohusiana na usanifu wa majengo fulani kama ilivyotakikana kisheria. Ni lazima washirikiane na mtaalamu wa majengo aliyesajiliwa nao wamiliki wa majengo lazima wahakikishe uzoaji wa taka kutoka kwa majengo yao unazingatia utaratibu,” ilisema notisi iliyotiwa saini.

Wamiliki wa majengo wanatakiwa pia kutengeneza njia mbadala ili kurahisisha kuingia kwa Watu Wenye Ulemavu (PWDs) madukani na kuwka kamera za CCTV ili kuimarisha usalama na kuhakikisha sehemu ya ardhi yao imepandwa miti.

Kulingana na Gavana Jonathan Bii, mji wa Eldoret ambao ni kitovu cha viwanda cha North Rift umetimiza mahitaji mengi ya hadhi ya jiji na kunufaika na ufadhili wa ziada kutoka kwa serikali ya kitaifa ili kuwavutia wawekezaji nchini na kimataifa kuanzisha biashara katika eneo hilo.

  • Tags

You can share this post!

Raia wa Gaza wapitia mateso ya kutisha hospitali zote...

ODM kutuza watakaozuia wakazi kujiunga na UDA Nyanza

T L