• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
Majeshi pinzani ya Somalia yakabana

Majeshi pinzani ya Somalia yakabana

Na MANASE OTSIALO

SHUGHULI za kibiashara Jumatatu zilivurugwa katika mji wa Mandera baada ya mapigano kuchacha kati ya makundi mawili ya kijeshi kutoka taifa jirani la Somalia.

Majeshi ya Somalia chini ya utawala wa Rais Mohammed Abdullahi Farmaajo na wale wa Jubbaland ambao wanaonyesha uaminifu kwa Rais Ahmed Madobe, walikabiliana katika mji wa Bulahawa karibu na mji huo wa mpakani.

Wanajeshi wa Somalia ambao wana makao yao jijini Mogadishu wamekuwa wakipiga kambi katika mji wa Bulahawa tangu Machi mwaka jana, baada ya kuwatimua wanajeshi wa Jubbaland kutoka mji huo.

Pia wamekuwa wakimsaka Waziri wa Usalama wa Jubbaland Abdirashid Hassan Abdinur maarufu kama Abdirashid Janan ambaye amekuwa mafichoni katika mji wa Mandera.

Tangu wakati huo, Bw Janan amekuwa akijipanga ili kuteka mji huo wa Bulahawa ambao si mbali na mji wa Mandera. Amekuwa akipokea silaha kutoka Kismayu na kuimarisha kikosi chake cha jeshi kabla ya mashambulizi ya Jumatatu.

Kwa siku yote, biashara nyingi zilisalia kufungwa mjini Mandera kutokana na makabiliano kati ya wanajeshi hao huku akina mama na watoto wakitorokea usalama wao kwenye mji wa Sufti ambao upo mpakani mwa Kenya na Ethiopia.

“Siwezi kukubali kubaki hapa nife. Nakimbilia usalama wangu pamoja na watoto wangu Ethiopia hadi hali ya utulivu irejee,” akasema Bi Halima Alio.

Mnamo Novemba 2020 Rais Farmaajo alishutumu Rais Uhuru Kenyatta kwa kuandaa mkutano na Rais Madobe, akishikilia kwamba Kenya ilikuwa ikimsaidia kiongozi huyo kijeshi ili kuvuruga amani na utawala wake nchini Somalia.

Kenya haikujibu madai hayo japo Rais Farmaajo aliwaongeza wanajeshi wake wa kutoa ulinzi mpakani hasa katika mji wa Bulahawa. Ingawa mji huo ulitwaliwa na wanajeshi wa Somalia, utawala wa Jubbaland umekuwa ukiweka mikakati ya kuudhibiti tena kupitia mashambulizi makali ya kivita.

Hata hivyo, Kenya imekuwa ikimsaidia Bw Janan na hayo yalidhihirika mnamo Machi mwaka jana, wanajeshi wa KDF walipomhamisha kutoka Mandera hadi Kapedo, viungani mwa mji huo kutokana na sababu za kiusalama.

Baadaye alihamishwa pamoja na kikosi chake cha walinda usalama kutoka Kapedo hadi eneo la Omar Jillo baada ya baadhi ya viongozi wa Kaskazini Mashariki kulalamikia uwepo wake mjini Mandera.

Duru ziliarifu kwamba wanajeshi wa Jubbaland walifanya mashambulizi ya kushtukiza na wakafaulu kuwafurusha wenzao wa Somalia kisha kutwaa udhibiti wa mji wa Bulahawa kwa mara nyingine.

Wanajeshi wa KDF ambao wamekashifiwa kwa kupendelea Jubbaland nao walikuwa ange mjini Mandera huku wakionekana kuwa tayari kukabiliana na mashambulizi yoyote.

Pia ni wanajeshi hao wa KDF ndio waliwaleta wanajeshi wa Jubbaland waliojeruhiwa kupokea matibabu katika hospitali ya rufaa ya Mandera.

You can share this post!

MARWA: Chipukizi anayelenga kufikia hadhi ya Lupita...

RIZIKI: Funzo la Covid-19 katika suala la ajira