• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Makazi ya Askofu wa Kanisa la Methodist yabomolewa Kilifi

Makazi ya Askofu wa Kanisa la Methodist yabomolewa Kilifi

NA ALEX KALAMA

MAAFISA wa Polisi katika Kaunti ya Kilifi wameanzisha uchunguzi baada ya makazi ya Askofu wa Kanisa la Methodist lililoko mjini Kilifi, kuvunjwa mnamo Jumapili jioni na watu wanaosemekana kuwa wafuasi wa kanisa hilo, ambalo liligawanyika mwaka 2019 baada ya baadhi ya wafuasi kulitaka kanisa hilo kugatuliwa.

Kulingana na Askofu Peter Mwavuo Karisa, mali ya thamani isiyojulikana iliharibika kutokana na ubomoaji huo ambao ulifanywa kwa kutumia tingatinga la bomoabomoa, ambalo liliingia katika uwanja wa kanisa licha ya kuwepo kwa askari aliyekuwa akilinda eneo hilo.

Bw Karisa anadai kwamba askari aliyekuwa akilinda makazi hayo alisema mwenyekiti wa kanisa hilo alikuwepo shughuli ya ubomoaji ikiendelea.

Ubomoaji huo ulifanyika wakati ambapo kesi inayohusu Kanisa la Methodist katika Kaunti ya Kilifi kutaka kujisimamia na kuondolewa chini ya usimamizi wa afisi za Nairobi iko mahakamani.

Sehemu mojawapo ya Kanisa la Methodist mjini Kilifi. PICHA | ALEX KALAMA

Hali inaonekana kuwa mbaya zaidi baada ya kundi linalotaka kujitenga kudaiwa kuchukua hatua na kuingia ndani ya uwanja wa Kanisa chini ya usimamizi wa askari gongo na kubomoa makazi ya kasisi aliyekuwa amesafiri hadi Kikambala kwa shughuli za kikazi.

“Swala kama hili kufanywa na watu ambao wanaitwa Wakristo ni jambo la kusikitisha sana. Sisi kama tumeitwa ndio nuru ya ulimwengu na yale mambo ambayo tunatakiwa tuangazie ulimwengu yanaonekana kuwa ni giza basi kanisa linakosa maana kabisa,” akasema Bw Karisa.

Mama Mwinjilisti Agnes Kabuka ameonekana alighadhabishwa na tukio hilo akieleza kuwa makazi hayo yalijengwa na fedha za waumini kuanzia mwanzo hadi kukamilika kwake.

“Kanisa hili liligawanyika… lina makundi mawili ambapo sasa kundi lile la pili ndilo halimtaki askofu. Ninahuzunija moyoni kwa sababu hii nyumba ni ya Sinodi nzima ya Kilifi, tena kujengwa kwake ni sisi wanaSinodi tuliochimba msingi,” alisema Bi Kabuga.

Askofu Mwavuo naye vile vile ameelezea masikitiko yake na kuwashauri Wakristo kukumbatia amani badala ya malumbano.

“Sisi Wakristo tunafaa kuwa kielekezo cha mambo mema kwa jamii. Sasa ikiwa tutakosana na kuvurugana, ni yupi ambaye atakumbatia amani? Ni aibu kubwa kwamba hili limetokea,” alisema Bw Karisa.

  • Tags

You can share this post!

Mswada wa Fedha, 2023: Raia roho mkononi

AMINI USIAMINI: Tandu wanaofahamika kama Giant centipedes

T L