• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:50 AM
MALENGA WA WIKI: Ali Mtenzi, mshairi stadi anayetamba pia katika uanahabari

MALENGA WA WIKI: Ali Mtenzi, mshairi stadi anayetamba pia katika uanahabari

Na HASSAN MUCHAI

JUMA Ali Mtenzi aliyejulikana awali kama Maskini Jeuri na baadaye Ustadh Mtenzi ni mshairi na mwanahabari shupavu anayetambuliwa kote nchini.

Mtenzi amekuwa mwanahabari ambaye amewahi kuhudumu katika vituo kadhaa vya habari vikiwemo NTV, KTN, Citizen, BBC na hatimaye K24.

Lakabu yake ya kwanza ya Maskini Jeuri ilitokana na ubishi mkali baina yake na mshairi fulani. Aliachana na lakabu hiyo na kujipa Ustadhi Mtenzi kama njia moja ya kumpa heshima babu yake Jama Ali aliyetambulika sana mjini Mombasa kutokana na kazi zake za ushairi.

Mtenzi anajulikana sana na wapenzi wake kutokana na vipindi vyake alivyopeperusha kupitia idhaa za KTN, Citizen na K24.

Vipindi hivyo vya kuchekesha ambavyo ni Heka heka za wiki (Citizen) Kukuru kakara za kisiasa (KTN) na Sokomoko (K24) alivipeperusha kila Ijumaa jioni kuonyesha matukio na vitimbi vya wanasiasa kila wiki. Vilikuwa maarufu sana na kupata uungwaji mkubwa wa mashabiki.

Bali na kazi za uanahabari na hasa utangazaji, Mtenzi ni mwandishi shupavu wa makala aina mbali mbali yanayosimulia maisha ya jamii.

Talanta yake na uzoevu wake katika kazi hii umemfanya kupogombewa na mashirika mengi ya habari.

Hata hivyo, kwa sasa anasema, angependa kutulia kwanza hadi atakapopata mwajiri mzuri atakayejali maslahi .

Hivyo, yeye huchukua muda mwingi kurekodi vipindi ambavyo kupitia kampuni yake ya habari na kuviweka kwenye mitandao ya kijamii ambako vinapendwa sana.

Mtenzi anafahamu fika jukumu lililo mbele yake la kuelimisha, kuburudisha na kuikoosa jamii yake.

Kupitia kitabu chake cha tamthilia ni rangi tu kilichochapishwa na shirika la Oxford University mwaka 2013, Mtenzi ametumia mbinu hii kutetea jamii ya zeruzeru. Anasema zeruzeru ni watu kama wengine licha ya tofauti za rangi ya ngozi yao.

Tamthilia hiyo iliyopokewa vyema masokoni, imeuza zaidi ya nakala 700,000. Anatumai kuwa itafanya zaidi miaka inayofuata.

Bali na tamthilia, Mtenzi ana miswada mingine ya uandishi ambayo anasubiri kuiwasilisha kwa wachapishaji siku za usoni. Ametunga zaidi ya mashairi 2000 na anatumai kuwa na diwani yake mwenyewe.

Ushairi: Mtenzi anaamini ushairi wake unatokana na kipawa alichorithi kutoka kwa babu yake mzee Jama Ali.

Ni babu yake aliyemfunza kunga za ushairi na kumhamasisha kujitosa kikamilifu kwenye fani hii. Mazingira aliyokulia mjini Mombasa yalichangia pakubwa sana kuathiri lugha yake na kumfanya kupenda fani hii.

Anasema nyakati zao kulikuwa na tafrija na ngoma mbali mbali za uswahili zilizojenga hisia zake kupenda kutunga mashairi. Alitangamana na wenyeji wa Mombasa na kila mara akivutiwa na fani hii.

Mtenzi alizaliwa 1968 mtaani Majengo Mombasa. Mtenzi ni miongoni mwa wa kutoka kabila dogo la Wachangamwe wanaozungumza Kichangamwe ambacho ni mojawapo ya lahaja za Kiswahili.

Alianza masomo yake katika Shule ya Msingi ya Makupa Catholic kabla ya kuhamia New Era na Kilindini kwa masomo ya upili. Hatimaye alijiunga na Chuo cha Professional Studies kwa somo la uhasibu.

Ingawa Mtenzi amesomea uhasibu na kuhitimu vyema, tamaa yake tangu utotoni ilikuwa kuhudumia umma kupitia uandishi na zaidi uanahabari.

Akiwa mdogo, alitamani kuwaiga watanagzaji waliovuma nyakati hizo kama Leonard Mambo Mbotela, Mohammed Juma Njuguna miongoni mwa wengine.

Akiwa Makupa, aliwashangaza walimu wake kwa ubunifu wake wa hali ya kutunga kutunga na kughani mashairi.

You can share this post!

JAMVI: Mtihani wa kuuza Muturi kama mrithi wa Uhuru Mlimani

Rais apanga kuunda miungano ya amani