• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 10:55 AM
Manufaa tele ya ufugaji nyuki wanayoridhia baada ya kuokoa msitu

Manufaa tele ya ufugaji nyuki wanayoridhia baada ya kuokoa msitu

NA SAMMY WAWERU

MSITU Kirisia, ulioko Maralal, Samburu wakati mmoja ulikuwa umevamiwa na maskwota wa ndani kwa ndani. 

Jamii inayoishi humo ikiwa ni wafugaji wa kuhamahama, walikuwa wameunda manyatta – makazi maalum, miti ikaangushwa, baadhi wakiingilia shughuli ya uchomaji makaa na kilimo.

Maliasili iliharibiwa, msitu uliokuwa chanzo cha chemichemi za maji na mvuto wa mvua ukawa hauna thamani tena.

Hawakujua hatua walizochukua zitawageuka, mifugo wakakosa malisho na maji, mzozano wa wanyamapori na binadamu, na wenyewe kwa wenyewe ukawa ratiba ya kila siku wakisaka chakula.

Ukame, maarufu kama Jilal Kisamburu ukawacharaza.

Kulingana na Douglas Leboiyare, Mwenyekiti wa Muungano wa Kijamii Kuhifadhi Msitu Kirisia (KCFA) ulioanzishwa 2018, wenyeji walitathmini athari zilizowakumba na kubaini suluhu ilikuwa miongoni mwao wenyewe.

“Tulijiuliza, kwa nini tuhangaishwe na ukame ilhali tuna maliasili ya kutosha?” ahoji.

Desemba 2020 walianza oparesheni kuondoka Mlima Kirisia, uliokuwa umevamiwa na zaidi ya maskwota 5, 000.

Msitu huo wenye ukubwa wa Hekta 92, 000 unamilikiwa na serikali.

“Awali, serikali ilikuwa imejaribu kuondoa wavamizi na haikufua dafu. Haikuwa rahisi, ila tulikuwa tumeamua liwe liwalo lazima watu waondoke,” aelezea.

Chini ya Mpango kunusuru msitu huo, KCFA kwa ushirikiano na Shirika la Muungano wa Umoja wa Kimataifa la Chakula na Kilimo (FAO), Shirika la Huduma za Misitu (KFS) na lile la Wanyamapori (KWS), Kenya Water Towers, na wadauhusika wengine, muungano huo umefanikiwa kuukoa.

Mwakilishi FAO Kenya, Balozi Carla Mucavi (kulia) na Mwenyekiti KCFA, Douglas Leboiyare wakijadiliana. PICHA | SAMMY WAWERU

Vyanzo vya maji vya msituhai huo, chemichemi, vimerejea.

Ni afueni ambayo imejiri na manufaa tumbi nzima, kando na kupata nyasi za mifugo wakazi wakiingilia shughuli za ufugaji nyuki.

“Tumeweka sheria kali, hakuna ujenzi wa majengo, uchomaji makaa, kukata miti wala kuendeleza kilimo kwenye msitu. Moran hulisha mifugo wakiwa na jukumu la kuulinda,” asema Leboiyare.

Isitoshe, wafugaji kutoka maeneo kame (ASAL) jirani hasa Laikipia, Samburu Mashariki na Kaskazini wanategemea msitu huo.

Naramat CFA, ni mojawapo ya chama kinachounda KCFA chenye zaidi ya watu 2, 000 walio na mradi kufuga nyuki.

Aidha una mizinga 150, wanachama vilevile wakiwa na mingine kwenye mashamba yao.

“Maua yanapochana, juisi yake ni chakula cha nyuki na tumeigeuza kuwa pato la ziada kuwafuga na kurina asali,” asema John Lelesit, mwenyekiti wa ufugaji nyuki katika chama hicho.

Lelesit kando na kuwa mfugaji wa ng’ombe wa maziwa, anaambia Akilimali kwamba anamiliki mizinga 100.

Msitu Kirisia unalindwa na askari wa akiba, chini ya Naramat wakitegemea ufadhili wa wahisani na wasamaria wema.

“Tuna kitalu cha miche, ambayo wafadhili hununua kisha wanatupa kuipanda msituni,” adokeza Zeinab Leboiyare mmoja wa maskauti na askari wa akiba.

Zeinab pia ni mfugaji nyuki.

Chama cha Ushirika, Samburu Beekeepers Cooperative Society Ltd huwasaidia kusaka soko.

“Huongeza asali thamani tunapovuna, na kututafutia wanunuzi,” asema Silverna Lenturkan, mwenyeji anayemiliki mizinga 20.

Silverna Lenturkan, mmoja wa wafugaji nyuki Maralal, Laikipia akionyesha asali aliyorina. PICHA | SAMMY WAWERU

Kilo moja ya asali huuza Sh800.

Kupitia chama hicho cha ushirika, wamepata mafunzo kuongeza thamani bidhaa za nyuki, kama vile nta kutengeneza mishumaa, sabuni na mafuta ya kujipodoa.

Oktoba mwaka huu, FAO ilizawadi KCFA tuzo la kimaita kufuatia jitihada zake kutunza na kuhifadhi Msitu Kirisia.

“Kirisia imeashiria misitu mingine nchini iliyovamiwa pia inaweza kuokolewa, tunusuru mazingira,” asema Balozi Carla Mucavi, Mwakilishi FAO Keny.

Mikakati kuangazia tabianchi Barani Afrika, ikiwemo upanzi wa miti kwenye misitu ya umma ni kati ya ajenda zinazojadiliwa katika Kongamano la Tabianchi, COP27 linaloenendelea nchini Misri.

  • Tags

You can share this post!

Uhuru amfaa Ruto kimataifa na nchini

Uchaguzi wa wabunge wa EALA kufanyika kesho saa tatu na...

T L