• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:50 AM
Marcus Rashford apewa malengo ya kufungia Man-United mabao 20 katika EPL msimu huu wa 2022-23

Marcus Rashford apewa malengo ya kufungia Man-United mabao 20 katika EPL msimu huu wa 2022-23

MANCHESTER, Uingereza

KOCHA Erik ten Hag amemwekea fowadi Marcus Rashford malengo ya kupachika wavuni mabao 20 msimu huu ili kusaidia Manchester United kuhimili ushindani mkali kutoka kwa wapinzani wakuu kwenye kipute cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Kwa mujibu wa Ten Hag, idadi kubwa ya wanasoka wake wanahisi kuwa kikosi cha Man-United huwa tishio kubwa zaidi kwa wapinzani kila mara Rashford anapowajibishwa katika safu ya mbele na supastaa Cristiano Ronaldo kuwekwa benchi.

Kufikia sasa, Rashford, 24, amefungia Man-United mabao matatu na kuchangia mengine mawili. Hiyo ni ishara ya kuimarika kwake ikizingatiwa kuwa alipachika wavuni magoli matano na kutoa krosi mbili zilizozalisha mabao msimu uliopita wa 2021-22.

“Rashford analenga kuwa sehemu ya kikosi kitakachochezea Uingereza kwenye fainali zijazo za Kombe la Dunia nchini Qatar. Amefufua makali yake na ndiye atakuwa fowadi tegemeo katika safu ya mbele ya Man-United,” akasema Ten Hag.

“Ana uwezo mkubwa wa kuwa miongoni mwa wanasoka bora zaidi duniani na tayari amedhihirisha hilo kwa matokeo ya kuridhisha kwenye mechi chache za muhula huu. Inawezekana atufungie mabao 20 na kusaidia kikosi kutwaa taji la EPL,” akaongeza kocha huyo raia wa Uholanzi.

Man-United waliofungiwa mabao mawili na Rashford katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Arsenal mnamo Septemba 4, 2022 ugani Old Trafford, sasa wanakamata nafasi ya tano kwenye jedwali la EPL kwa alama 12, mbili pekee nyuma ya Tottenham Hotspur na mabingwa watetezi, Manchester City. Ni pengo la pointi tatu ndilo linawatenganisha na Arsenal wanaoselelea kileleni kwa pointi 15, mbili zaidi kuliko nambari nne Brighton.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Neymar sasa ni wa nne katika orodha ya wafungaji bora wa...

CHARLES WASONGA: IEBC: Kenya Kwanza isiadhibu...

T L