• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Mashamba bado donda sugu Kenya kwa miaka 58 ya uhuru

Mashamba bado donda sugu Kenya kwa miaka 58 ya uhuru

Na SAMMY WAWERU

MIAKA 58 baada ya Kenya kupata uhuru wa kujitawala, umiliki wa mashamba umekuwa tatizo kubwa katika maisha ya kisiasa, uchumi na kijamii kwa Wakenya.

Kulingana na wasomi, viongozi waliochukua madaraka kutoka kwa wakoloni ndio waliweka msingi wa matatizo ya muda mrefu kuhusu mashamba.

Kulingana na Prof Philip Onguny na Taylor Gillies wote wa Chuo Kikuu cha Saint Paul nchini Canada, kwenye ripoti yao mnamo 2019, mabwenyenye waliopokezwa madaraka na mzungu waliteka haki za kumiliki mali, na kuanzia hapo haki za wananchi wa kawaida kuhusu umiliki wa mali na hasa mashamba zikaanza kuvunjwa kiholela.

“Ardhi iliyokuwa imenyakuliwa na walowezi hasa Waingereza ilitwaliwa na utawala wa Mzee Jomo Kenyatta, na ikauzwa kwa washirika wake.

“Mwenendo huo uliendelea chini ya utawala wa Daniel arap Moi, ambaye alikuwa akigawa ardhi kiholela kwa maslahi ya kisiasa,” wasema wasomi hao.

ARDHI NA SIASA

Wanaeleza kuwa suala la ardhi liligeuzwa kuwa la kisiasa, na hakuna utawala ambao umekuwepo tangu 1963 umeonyesha nia ya kufanya marekebisho ya kuwapa Wakenya haki zaidi za kumiliki ardhi.

“Sababu kuu ya viongozi kukataa marekebisho katika usimamizi wa ardhi ni kuwa suala la mashamba lina mshikamano mkubwa na siasa, hasa miongoni mwa mabwanyenye walio madarakani,” Prof Onguny na Gilleis wanaeleza.

Wachanganuzi wanasema kuwa dosari za muda mrefu kuhusu umiliki wa ardhi ndizo kiini kikuu cha ghasia za mara kwa mara za kikabila hasa maeneo ya Rift Valley, pamoja na umaskini mkubwa ambao umesambaa kote nchini.

“Wanasiasa wamekuwa wakitumia udhaifu wa mfumo wa ardhi kuchochea ghasia kwa manufaa yao ya kisiasa, kwa mfano ghasia zilizozuka mnamo 1992, 1997 na 2007,” Prof Onguny na Gillies wanaeleza.

Kulingana na Ripoti ya Ndung’u iliyoandaliwa mnamo 2004, ardhi imekuwa kifaa cha kutumiwa na viongozi kuchochea uadui wa kikabila na unyakuzi wa ardhi ya umma kama vile misitu kwa maslahi ya kibinafsi na kisiasa.

Msomi Jacquiline Klopp wa Chuo Kikuu cha Columbia nchini Amerika anasema: “Misingi ya taifa la Kenya imejengwa katika unyakuzi wa ardhi, na hivyo ni sawa mtu akisema kuwa unyakuzi wa ardhi ni wa rika moja na Kenya yenyewe.”

  • Tags

You can share this post!

‘Kiwango cha maambukizi ya corona kinaendelea...

Chelsea tayari kumsajili Romelu Lukaku kutoka Inter Milan