• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 3:34 PM
Mashujaa Dei: Hoteli za Kericho na kaunti jirani zavuna mihela biashara ikinoga

Mashujaa Dei: Hoteli za Kericho na kaunti jirani zavuna mihela biashara ikinoga

ELIZABETH OJINA Na CHARLES WASONGA

MAKALA ya 60 ya Mashujaa Dei ni kesho Ijumaa, Oktoba 20, 2023, ambapo Kaunti ya Kericho ndiyo itakuwa mwenyeji.

Hii ni fursa kwa biashara za hoteli kunoga katika kaunti hiyo, huku ikitarajiwa kwamba wageni wengine watatafuta malazi katika hoteli za kaunti jirani ya Kisumu.

Tayari hoteli za hadhi ya juu Kericho na Kisumu zimejaa kwa asilimia 90 ikiwa ni siku moja kabla ya siku ya siku.

Hafla ya kitaifa itaandaliwa katika uwanja wa Kericho Green ambapo Rais William Ruto anatarajiwa kuwaongoza Wakenya kujivunia juhudi za mashujaa waliopigania uhuru na wengine wanaoendelea kuiletea nchi sifa.

Hoteli ambazo tayari zimejaa ni Sunshine, Exotic House, Tiddys, Sahara Gardens, Tea Hotel, na Golf Club. Hizi zote ziko katika Kaunti ya Kericho.

Meneja wa hoteli ya Sunshine Bw Alphonce Otieno ameambia Taifa Leo hoteli hiyo imejaa hadi Oktoba 21, 2023.

“Hii asubuhi tumealika wanahabari kwa staftahi ambapo watu 400 watafika. Waliofika ni baadhi ya viongozi watakaohudhuria sherehe hizo za Mashujaa hapa Kericho,” amesema Bw Otieno.

Mwakilishi wa Muungano wa Wadau wa Sekta ya Utalii katika kanda ya Ziwa Victoria upande wa Kericho na Bomet Franklin Kirui ameelezea matumaini yake kwamba hoteli za South Rift zitauza chakula na vinywaji kwa wingi na pia zitavuna kutokana na huduma za malazi.

“Hoteli nyingi hapa zimejaa kwa hadi asilimia 100 kuanzia leo na hali itakuwa hivyo hadi Oktoba 21. Lakini kizuri kwa wadau ni kwamba ada imepandishwa kwa sababu ya utashi wa huduma,” akasema Bw Kirui.

Mbali na Kisumu, wageni wengine pia wataenda Bomet.

Hoteli ambazo zinavuna Kisumu ni Sarova Imperial, Acacia Premier, na Best Western.

Rais wa Angola Joao Manuel Gonclaves Lourenco atakuwa miongoni mwa wageni kutoka ng’ambo watakaohududhuria sherehe ya kitaifa ya Mashujaa.

Balozi wa Angola nchini Sianga Abilio alitangaza hilo Alhamisi, Oktoba 5, 2023, alipomtembelea Gavana wa Kericho Dkt Eric Mutai afisini mwake, mjini Kericho.

“Ni furaha yangu kukueleza kwamba Rais wangu Mheshimiwa Joao Manuel atakuwa mgeni mheshimiwa na yu tayari kuunga na wakazi wa Kericho na Wakenya wengine wakati wa sherehe za Mashujaa Dei,” akasema Balozi Abilio.

Kwenye kikao na wanahabari, Gavana Mutai alisema walizungumza kuhusu nafasi mbalimbali ya kibiashara yenye faida kwa kaunti ya Kericho na Angola yenye utajiri mkubwa wa mafuta. Mkuu huyo wa kaunti alisema kuwa Kericho inaweza kuuza majani chai moja kwa moja nchini Angola.

“Baada ya kumtembeza katika uwanja huu wa michezo, balozi alifurahishwa na matayarisho ya kuandaa sherehe hizo na akaahidi kuleta ujumbe mkubwa kutoka Angola kufurahia mazuri katika kaunti yetu,” akaongeza Dkt Mutai.

  • Tags

You can share this post!

Brazil wafinywa na Uruguay, Messi aibeba Argentina kwa...

Kaburi la bahati nzuri lavutia watalii kutoka pembe zote za...

T L