• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
Matumaini Achani huenda akapeperusha UDA Kwale

Matumaini Achani huenda akapeperusha UDA Kwale

Na SIAGO CECE

NAIBU Gavana wa Kaunti ya Kwale, Bi Fatuma Achani, amepata nafasi bora ya kushinda tiketi ya Chama cha United Democratic Alliance (UDA), kuwania ugavana mwaka ujao, baada ya mpinzani wake kujitenga na chama hicho.

Bw Lung’anzi Mangale, ambaye alikuwa ametangulia kutangaza nia yake ya kushindania tiketi hiyo, sasa amejitenga na UDA baada ya Naibu Rais William Ruto kuashiria anampendelea Bi Achani.Wakati Dkt Ruto alipozuru Pwani wiki chache zilizopita, alimsifu Bi Achani na kusema anastahili kupewa nafasi ya kuendeleza kazi zilizoanzishwa na Gavana Salim Mvurya, ambaye atakamilisha kipindi cha pili cha ugavana mwaka ujao.

Kabla ya ziara hiyo, Bi Achani alikuwa hajatangaza chama ambacho angetumia kuwania ugavana mwaka ujao, na alikuwa akisisitiza bado yeye ni mwanachama wa Jubilee.“Kwa sasa ninaweka juhudi zangu kujenga upya sifa zangu kibinafsi.

Sitaki ugombeaji wangu uhusishwe na chama chochote,” Bw Mangale alisema, kwenye mahojiano na Taifa Leo.Duru zilisema kuwa, alikataa ombi la baadhi ya wabunge wanaounga mkono Chama cha UDA huko Kwale kuwania kiti cha useneta.

Wakati wa ziara Dkt Ruto katika Kaunti hiyo, mwanasiasa huyo alisimama katika jukwaa moja na Bi Achani, lakini ni jukwaa hilo ambalo Dkt Ruto alimuidhinisha Bi Achani akisema kuwa “Kazi iendelee”.Bw Mangale sasa amepuuza ushirikiano wake wa awali na UDA.

“Kuzungumza kwangu kwenye mkutano wa Naibu wa Rais hakumaanishi jambo lolote kubwa. Nimeridhika tu kwamba niliruhusiwa kuhutubia umati mkubwa kama huo,” alisema Bw Mangale. Wanakamati wa kikosi chake cha kampeni, pia walitoa malalamishi kuwa Bw Mangale hakupewa kiti jukwaani wakati wa ziara ya Naibu Rais, huku Bi Achani akikaa kando ya Dkt Ruto.

Bi Achani ambaye alichaguliwa 2013 na 2017 pamoja na Bw Mvurya, aliandamana na Dkt Ruto katika mikutano mbalimbali ya hadhara nje ya Kwale kama vile eneo la Malindi, Kaunti ya Kilifi, huku wawaniaji wengine wa UDA na wabunge wakimpigia debe kumrithi Bw Mvurya.

Yeye ni mmoja wa wanawake watatu Pwani, ambao wanataka kuwania ugavana kupitia kwa UDA, kando na Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa (Kilifi) na Bi Umra Omar (Lamu).Kando na wawili hao, kiti cha Bw Mvurya kinamezewa mate na wanasiasa wengine wanne kutoka vyama tofauti akiwemo Spika wa Bunge la Kaunti ya Kwale, Bw Sammy Ruwa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Prof Hamadi Boga, mfanyabiashara Daniel Dena na aliyekuwa waziri na balozi, Bw Chirau Ali Makwere.

Licha ya kuwa Dkt Ruto alihakikishia wafuasi wa UDA kutakuwa na kura ya haki kwenye mchujo, anakabiliwa na hali hiyo hiyo katika kaunti nyingine ambapo tiketi ya UDA inatafutwa na viongozi mbalimbali ilhali anaonekana kupendelea wanasiasa fulani.

You can share this post!

Wakurugenzi wa kampuni ya kuuza sukari wako na kesi ya...

IEBC huru kuandaa uchaguzi- Korti

T L