• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:55 AM
MATUNDURA: Athari za sera ya udhibiti kwa waandishi wa fasihi Afrika Mashariki

MATUNDURA: Athari za sera ya udhibiti kwa waandishi wa fasihi Afrika Mashariki

NA BITUGI MATUNDURA

Kwa majuma sita, msururu wa makala yangu umekuwa ukiangazia suala la udhibiti wa maandishi. Tayari nimekwisha kuangazia sura, aina za udhibiti na tajriba za baadhi ya waandishi tuliowateua, inabainika wazi kwamba athari za udhibiti wa maandishi au fasihi zinaweza kuwa ama chanya au hasi. Athari hasi ni pamoja na zifuatazo.

Mara nyingi aghalabu waandishi hulazimika kukimbilia uhamishoni ili kuokoa maisha yao. Kati ya waandishi ambao tumekwisha kujadili tajriba zao, imebainika wazi kwamba Ngugi wa Thiong’o, Alamin Mazrui, Abdilatif Abdalla walilazimika kukimbilia uhamishoni.

Waandishi vile vile wanaweza kuogopa kuandikia masuala nyeti au ya kisiasa na hivyo basi kuishia kuandika fasihi chapwa au masuala ya kimapenzi.

Katika mfumo wa kibepari, udhibiti wa fasihi unaweza kuwafanya waandishi kutungia masuala ya kimapenzi kwa misingi kwamba ukachero huwa umedumishwa. Mwandishi asiyetii matakwa ya serikali jinsi ambavyo tumeona anaweza kunyanyaswa.

Kuhusu suala hili, Maillu kwa mafano anasema : Mnamo 1973, kwenye jaribio la kuwafurahisha wasomaji wangu, nilichapisha kitabu changu kinachoitwa My Dear Bottle, ambacho kilionekana tu kuwa sarakasi.

Kwa hakika, msukumo wa kukiandika kitabu hicho ulitokana na shairi nililokuwa nimeliandika lenye anwani “Mathare Valley.”[…]Nilitaka kuikosoa serikali. […] Nilikuwa nimelituma shairi hilo lichapishwe kwenye gazeti la Nation, lakini likarejeshwa kwangu na maoni ya mhariri kwamba: “Ikiwa tutachapisha shairi hili, serikali ya Kenyatta itakuadhibu na kampuni yetu itakuwa mashakani”.

Kwa hiyo, niliamua kumsawiri mhusika mkuu katika kitabu changu kuwa mtu mlevi na awe nyenzo ya kusema kwa niaba yangu […] iliwachukua kipindi kirefu maafisa katika serikali ya Kenyatta kugundua njama yangu ya kutumia kikaragosi kuwavutia wasomaji wangu bila kushukiwa na utawala wa Kenyatta. […] maafisa wa serikali walinipokonya ala yangu na kuiharibu.

Prof Ngugi wa Thiongo makubwa ya kusimulia kuhusu jinsi Kenyatta alivyoharibu ala yake kwa kumweka kizuizini […] Jinsi nilivyoendelea kuandika zaidi, ndivyo niligundua kwamba kuna masuala niliyoyaandikia ambayo yaliihangaisha Serikali.

Niligundua kwamba Serikali haikujali hata chembe nilipoandika kuhusu mawingu, ngono, Mungu na Viumbe Vyake, jinsi ya kupata pesa na kuoa wake wengi.

Kutokana na hoja ya Maillu, athari nyingine ya udhibiti ni pale ambapo waandishi hujipata wakitekeleza udhibiti wa kibinafsi (self censorship) jinsi ambavyo David Maillu alivyofanya.

Kulingana Maillu, kwa kuogopa rungu la dola, waandishi au watunzi hujipata wakitunga kazi ambazo hazikosoi serikali au watawala bali hujihusisha na masuala ‘mepesi’ kama vile mazingira ambayo hayafungamani moja kwa moja na siasa.

Udhibiti wa maandishi vilevile unaweza kuwa na athari chanya. Waandishi na wanaharakati wanaoandamwa na rungu la dola mara nyingi huvumbua mbinu za kiubunifu za kusimba (encode) kazi zao hivi kwamba inakuwa vigumu kwa Serikali kugundua uzito wa kazi hizo.

Tunaamini kwamba hali hii ndiyo iliyompa msukumo mwandishi Katama Mkangi kuandika riwaya zake mbili – Mafuta (1984 ) na Walenisi kwa muundo ambao ni wa kimafumbo. Riwaya hizi zinafanana kwa kuwa zinajihusisha kwa kiasi kikubwa na suala la kisiasa.

Kazi hizi zinachunguza jinsi mfumo wa kisiasa unaothibitiwa na tabaka la watu wachache unavyoweza kuathiri maisha ya waliotawaliwa kijamii, kiuchumi, kisiasa na hata kisaikolojia. Walenisi ni riwaya iliyoandikwa kwa mtindo wa fumbo.

[email protected]

You can share this post!

INDINDI: Rais atuonyeshe mfano bora katika kuthamini...

Wakazi Nairobi kuzidi kukosa maji

adminleo