• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 AM
Maumivu Tanzania bei ya mafuta ikipaa na kupita ya Kenya

Maumivu Tanzania bei ya mafuta ikipaa na kupita ya Kenya

GEORGE HELAHELA, MCL na CHARLES WASONGA

KIVUMBI kimetokea nchini Tanzania baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei mpya za mafuta zitakazotumika mwezi huu wa Septemba ambazo zimepaa huku maumivu zaidi yakiwa katika bei ya dizeli.

Katika taarifa kwa umma iliyotolewa Jumanne Septemba 5, 2023, usiku na Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Dkt James Mwainyakule imeonyesha kwamba kuanzia Jumatano Septemba 6 jijini Dar es Salaam petroli itauzwa Sh3,213 (Ksh191.02) na dizeli itauzwa kwa Sh3,259 (Ksh193.75).

Bei hizo zinamaanisha kwamba dizeli nchini Tanzania inauzwa ghali kuliko Kenya, ambapo bei yake kwa sasa ni Ksh174.67 huku petroli, Kenya ikiizidi na karibu Sh3 pekee kutokana na bei yake ya Ksh194.68.

Itakumbukwa kwamba nchini Kenya, bei za mafuta zilipanda kufuatia kuongezwa kwa ushuru kutoka asilimia nane hadi asilimia 16 kupitia Sheria ya Fedha 2023 ambayo ilichochea upinzani kuitisha maandamano makubwa.

Kesi ya kupinga nyongeza hiyo ingali mahakamani.

Bei hizo zinamaanisha kuwa katika Mkoa wa Dar es Salaam, petroli imeongezeka kwa Sh14 kutoka Sh3,199 ya Agosti huku dizeli ikiongezeka zaidi kwa Sh324.

Hata hivyo, kwa upande wa mikoa mingine yenye bandari zinazoshusha mafuta nchini pia bei ya mafuta imepaa; Mtwara kwa mwezi huu lita moja ya petroli itauzwa Sh3,285 ikiongezeka kutoka Sh3,271 na upande wa dizeli itauzwa Sh3,332 kutoka Sh3,008 mwezi Agosti.

Aidha, bei ya mafuta pia imepaa kwa Mkoa wa Tanga ambapo kwa sasa lita moja ya petroli itauzwa Sh3,259 kutoka Sh3,245 Agosti huku dizeli nayo ikiongezeka zaidi kutoka Sh2,981 Agosti hadi Sh3,305.

Kuhusu sababu za kupanda kwa mafuta, Mkurugenzi wa Ewura amesema gharama za uagizaji katika soko la dunia na maamuzi ya kisiasa ya nchi wazalishaji mafuta zimechochea ongezeko hilo.

“Mabadiliko ya bei za mafuta kwa Septemba 2023 yanatokana na kupanda kwa gharama katika soko la dunia kwa hadi asilimia 21, gharama za uagizaji wa mafuta hadi asilimia 62 ikilinganishwa na Agosti,”

“Pia, maamuzi ya kisiasa katika nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani (OPEC+) imekuwa chanzo,” akasema Bw Mwainyakule.

Hali kama hii ya kupanda kwa bei za mafuta ilitokea mwaka 2022 ambapo Serikali mnamo Mei 2022 iliweka ruzuku ya Sh100 bilioni katika bidhaa hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi ili kupoza bei yake. Na Januari 2023 iliiondoa ruzuku hiyo.

Nchini Kenya, mnamo Agosti 14, 2023, serikali ilidumisha bei za bidhaa za petroli ambazo zimetumika tangu Julai 14, 2023, baada ya kurejesha mpango wa kutoa ruzuku kwa bei za bidhaa hizo.

“Kwa hivyo, kuanzia Jumanne Agosti 15, 2023, bei za mafuta aina ya petroli, dizeli na mafuta taa hazitabadilia. Bei hizo zitasalia Sh194.68 kwa lita moja ya petroli, Sh179.67 kwa lita ya dizeli na Sh169.48 kwa lita ya mafuta taa jijini Nairobi kuanzia siku hiyo,” Mamlaka ya Kudhibiti Bei za Kawi na Bidhaa za Petroli (EPRA) ikasema kwenye taarifa iliyotumwa Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo Daniel Kiptoo.

Serikali ya Rais William Ruto ilikuwa imetupilia mbali mpango wa kutoa ruzuku kwa bei za mafuta kuanzia Mei 2023, hatua iliyochangia bei za bidhaa za petroli kupanda kwa hadi Sh13 kwa lita moja.

Kulingana na EPRA, kurejeshwa kwa ruzuku kwa bei za mafuta kunalenga kuwakinga Wakenya kutokana na makali ya kupanda kwa bei kulikochangiwa na kupanda kwa bei za bidhaa hiyo katika masoko ya kimataifa.

“Ili kuwakinga wateja kutokana na bei za juu za mafuta zilizochangiwa na kuongezeka kwa bei ya mafuta yanayoagizwa kutoka nje, serikali imeamua kutoa ruzuku kwa bei za mafuta katika kipindi cha Agosti-Septemba,” taarifa ya EPRA ikasema.

Hii ina maana kuwa chini ya mpango huu mpya, serikali itaziruzuku Kampuni za Kuuza Mafuta (OMCs) kwa kuweka mkakati wa kutoongeza bei za bidhaa za mafuta.

Ikiwa serikali haingetoa ruzuku, inadiriwa kuwa bei za petroli, dizeli na mafuta taa zingeongezeka kwa Sh7.33, Sh3.59 na Sh5.74, kwa lita moja mtawalia.

Hii ina maana kuwa bei ya lita moja ya petroli jijini Nairobi ingepanda kutoka Sh194.68 hadi Sh202.01.

Nayo bei ya dezeli ingapanda kutoka 179.67 kwa lita hadi 183.26 huku bei ya mafuta taa ikiongezeka kutoka Sh169.48 hadi Sh175.22.

Ongezeko hilo lingeibua malalamishi makubwa kutoka kwa raia kwa sababu lingechochea kupanda kwa gharama ya maisha hata zaidi.

  • Tags

You can share this post!

Mwalimu anayetembea na risasi mguuni kwa miaka 8

Worldcoin iliingiza Sh2.5 bilioni nchini bila ufahamu wa...

T L