• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Mayatima, maskini wachinjiwa ng’ombe 1,000 sikukuu ya Idd

Mayatima, maskini wachinjiwa ng’ombe 1,000 sikukuu ya Idd

WAWERU WAIRIMU na MOHAMED AHMED

WAISLAMU katika Kaunti ya Isiolo Jumatatu walisherehekea Sikukuu ya Eid-Ul-Adha kwa njia ya kipekee baada ya kuwachinja ng’ombe 1,000 kisha kuwapa maskini na mayatima nyama ya mifugo hiyo.

Ng’ombe hao walitolewa kama sadaka kwa Allah na Shirika la Diyanet Vakfi kutoka Uturuki kusherehekea sikukuu hiyo ya kuchinja. Shirika hilo pia liliwatoa ng’ombe 4,000 waliochinjwa katika kaunti za Mombasa, Mandera na Garissa.

Shughuli hiyo ilitoa nafasi ya ajira kwa vijana wengi ambao walitia mfukoni Sh500 kwa kila ng’ombe aliyechinjwa.

Wahisani kutoka Shirika la Kutetea Haki za Kibinadamu Isiolo na Wanawake Waislamu walisaidia kuhakikisha nyama hiyo inasambazwa kwa maskini na mayatima pekee.

Mkuu wa Diyanet Vakfi, Mucahid Dormaz alisema kwamba nyama hiyo pia ilisambazwa hospitalini na magereza ili wagonjwa na wafungwa pia washerehekee Eid-Ul- Adha ambayo inaashiria mwisho wa kutimizwa kwa nguzo muhimu ya Kiislamu, Hajj kwa mahujaji waliosafiri mjini Mecca nchini Saudia Arabia.

Wafungwa katika magereza ya Chuka katika Kaunti ya Tharaka-Nithi, Embu na Kangeta, Kaunti ya Meru ni kati ya walionufaika na ukarimu huo wa shirika la Diyanet Vakfi.

Kulingana na Bi Batula Ali, zaidi ya maboma 400 ya mayatima yalikuwa yamepokea nyama hiyo pamoja na wakongwe katika jamii.

Huku hayo yakiendelea, baadhi ya Waislamu katika maeneo mbalimbali nchini Jumapili walijaa nyanjani na misikitini kushiriki maombi ya Idd-ul-Adha.

Walioshiriki ibada za Jumapili waliasi tangazo la Kadhi Mkuu Ahmed Muhdhar kwamba sikukuu hiyo iadhimishwe jana.

Tangazo la Sheikh Muhdhar kwamba sherehe hizo ziandaliwe jana zilitegemea kuonekana kwa mwezi japo waliompuuza walizingatia matukio nchini Saudi Arabia ambapo mahujaji walisimama Arafa Jumamosi.

Vile vile alisema sherehe zilipaswa kuandaliwa siku iliyotangazwa na serikali kama sikukuu ya kitaifa.

“Hapa Kenya tulianza kufunga Agosti 3 ambayo ni siku ya kwanza ya mwezi wa Dhul-hijjah. Tunafaa kufungua baada ya siku ya tisa ambayo ni Jumatatu Agosti 12,” akasema Sheikh Muhdhar wiki jana.

Sikukuu ya Idd Ul Adha ambayo pia hufahamika kama Idd Ul Hajj huadhimishwa baada ya kukamilika kwa Hajj ambayo inaweka kwenye uhalisia kisa cha mtumishi wa Allah, Ibrahimu kutaka kumtoa mwanawe Ismail kafara kwa mungu ila badala yake akateremshiwa kondoo.

You can share this post!

Polisi wazima wakazi kuchota mafuta Nakuru

Wanafunzi waliotia fora tamashani kumtumbuiza Ruto

adminleo