• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
Mbappe abeba PSG dhidi ya Auxerre

Mbappe abeba PSG dhidi ya Auxerre

Na MASHIRIKA

PARIS Saint-Germain (PSG) walianza kunusia taji lao la 11 la Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) baada ya fowadi Kylian Mbappe kuwafungia magoli mawili katika ushindi wa 2-1 dhidi ya AJ Auxerre ugani Abbe Deschamps, Jumapili.

PSG, ambao ni mabingwa watetezi wa Ligue 1, sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 84, sita mbele ya nambari mbili Lens ambao pia wametandaza michuano 36.

Chini ya kocha Christophe Galtier, PSG wanahitaji sasa alama moja pekee kutokana na mechi mbili zilizosalia ligini msimu huu ili kujipa uhakika wa kuhifadhi ufalme wa Ligue 1. Watatia taji hilo kapuni wikendi hii iwapo wataepuka kichapo kutoka kwa Racing Strasbourg watakaomenyana nao Jumamosi, ugenini.

Mbappe, anayeongoza orodha ya wafungaji bora wa Ligue 1 kwa mabao 28, alicheka na nyavu mara mbili chini ya dakika nane za kipindi cha kwanza kabla ya Lassine Sinayoko kufuta machozi ya Auxerre mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Kufikia sasa, Mbappe, 24, ametikisa nyavu za wapinzani mara 40 na kutoa krosi zilizochangia mabao tisa kutokana na michuano 41. Mshambuliaji huyo raia wa Ufaransa amehusika moja kwa moja katika mabao 33 ambayo yamefungwa na PSG katika mechi 32 za Ligue 1 muhula huu.

PSG wamenyanyua mataji manane kati ya 10 yaliyopita ligini. Walifikia rekodi ya Olympique Marseille na Saint-Etienne ambao wametawazwa wafalme wa Ligue 1 mara nyingi zaidi walipoibuka mabingwa wa kipute hicho kwa mara ya 10 msimu jana.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Kenyatta: Ningali kiongozi wa Jubilee

Akaunti za Pasta Ezekiel Odero kufunguliwa

T L