• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
MBWEMBWE: Aisee Aubameyang si masihara, anasukuma mchuma wa dhahabu

MBWEMBWE: Aisee Aubameyang si masihara, anasukuma mchuma wa dhahabu

Na CHRIS ADUNGO

PIERRE-EMERICK Emiliano Francois Aubameyang, 30, ni mshambuliaji matata wa Arsenal na sogora wa kwanza raia wa Gabon kuwahi kusakata soka katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) wakati akivalia jezi za Borussia Dortmund.

Isitoshe, ndiye nyota wa kwanza katika klabu ya Dortmund kuwahi kufungua msimu kwa kupachika wavuni mabao matatu (hat-trick) katika mechi moja.

Anajulikana sana kutokana na kasi yake ya ajabu kila anapodhibiti mpira na anashikilia rekodi ya kukimbia hatua ya mita 30 kwa muda wa chini ya sekunde 3.7.

Ukwasi

Kwa mujibu wa Jarida la kimataifa la Forbes, thamani ya mali ya Aubameyang inakadiriwa kufikia Sh5 bilioni na kiini kikubwa cha utajiri wake ni mshahara wa Sh730 milioni aliokuwa akipokezwa na Dortmund kila mwaka kabla ya Arsenal kuzitwaa huduma zake kwa kima cha Sh8.4 bilioni mnamo Januari 2018.

Ndiye anayeongoza orodha ya wachezaji wakwasi zaidi nchini Gabon baada ya Mario Rene Junior Lemina wa Southampton na Alexander N’Doumbou anayeipigia Shanghai Shenhua ya China. Lemina kwa sasa anawachezea Galatasaray ya Uturuki kwa mkopo wa mwaka mmoja.

Mshahara wa Sh26 milioni ambao kwa sasa Aubameyang anatia kapuni mwishoni mwa kila wiki uwanjani Emirates, Uingereza unamfanya kuwa mchezaji wa pili baada ya Mesut Ozil ambaye anadumishwa kwa fedha za kiasi cha juu zaidi kambini Arsenal.

Ozil ambaye ni kiungo mzawa wa Uturuki na raia wa Ujerumani kwa sasa anaridhika na takriban Sh45 milioni kwa juma.

Mgongo wa Aubameyang kimshahara unasomwa kwa karibu na Alexandre Lacazette, Sead Kolasinac, Hector Bellerin na sajili mpya Nicolas Pepe, 24, aliyeagana na Lille ya Ufaransa mwishoni mwa msimu jana kwa kima cha Sh9.4 bilioni.

Mbali na mshahara wake mnono, Aubameyang hutia mfukoni kitita kikubwa cha fedha kutokana na dili za matangazo, kushiriki mazoezi na asasi mbalimbali, bonasi na marupurupu ya kushinda mechi katika ngazi za klabu na timu ya taifa.

Magari

Sawa na wachezaji wa haiba yake katika ulingo wa soka, magari anayoyaendesha Aubameyang huwaacha wengi vinywa wazi. Anamiliki Ferrari 458 yenye thamani ya Sh24.8 milioni, Aston Martin DB9 iliyomgharimu Sh18.4 milioni, 918 Spyder ya Sh72 milioni na Lamborghini Gallardo LP560-4 Matte itakayokulazimisha kuweka mezani Sh16.8 milioni ili kuipata.

Upekee wa gari hilo ni kwamba limeundwa kutokana na madini mengi ya dhahabu.

Majumba

Aubameyang anajivunia kasri la Sh700 milioni jijini London. Kuhamia Uingereza kuvalia jezi za Arsenal kulimweka katika ulazima wa kutupa mnadani nyumba yake nyingine ya Sh600 milioni iliyotwaliwa na kiungo Marco Reus, 30. Aubameyang ana majengo mengi ya kifahari katika miji tofauti nchini Gabon.

Mawili kati ya majumba yaliyo chini ya ‘milki’ yake ni yale aliyowajengea nduguze wawili kwa kima cha Sh140 milioni mnamo 2011. Kwa kuwa mahusiano kati yao yamejengeka kwa misingi ya mapenzi ya dhati, nduguze Aubameyang wamekuwa na mazoea ya kutua katika kila uwanja ambako Arsenal huchezea kwa minajili ya kumtilia shime.

  • Tags

You can share this post!

ULIMBWENDE: Epuka matumizi holela ya vipodozi

Gurudumu la ndege ya Silverstone Air ladondoka ikiwa imepaa

adminleo