• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Mgogoro Meru: Wapinzani wa Mwangaza sasa wageukiana

Mgogoro Meru: Wapinzani wa Mwangaza sasa wageukiana

NA GITONGA MARETE

MZOZO unatokota miongoni mwa wapinzani wa Gavana wa Meru, Kawira Mwangaza kuhusu namna ya kugawana nyadhifa iwapo watafanikiwa kumuondoa afisini.

Katibu Mkuu wa Chama cha Uwezeshaji Ugatuzi (DEP) Mugambi Imanyara Jumatatu alitoa onyo, akisema “Kawira si mbaya kama ulivyofikiria. Tuko na matapeli wabaya zaidi”.

DEP ndicho chama cha wachache katika bunge hilo chenye wanachama 21 huku chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) ndicho chenye wabunge wengi 22 katika bunge hilo lenye wanachama 69.

Kando na vyama hivyo viwili, vingine ambavyo vimeidhinisha mipango ya kuondolewa madarakani kwa gavana Mwangaza ni Party of National Unity (PNU), National Ordinary People Empowerment Union (NoPEU) Democratic Party na Vyama huru.

Katika mtandao wao wa kundi la WhatsApp, ‘Meru Progressive’ ambalo huwaleta pamoja wakazi na wataalamu wa Meru na Nairobi, maoni ya Bw Imanyara yalizua shutuma huku viongozi wa chama hicho wakimkana wakisema nia yake ni kuleta migawanyiko.

Maoni hayo yalijiri huku gavana huyo akitarajiwa kujua hatima yake leo (Jumatano) wakati wajumbe wa bunge la kaunti wana uwezekano wa kumwondoa mamlakani kwa kuwasilisha notisi ya hoja ya kumtimua.

Takriban wanachama 60 wa bunge hilo walikutana jijini Nairobi siku ya Jumapili katika juhudi za kuthibitisha misingi ambayo itategemewa kumwondoa afisini.

Bw Titus Ntuchiu, naibu kiongozi wa chama cha DEP alisema wanajaribu kutatua tatizo wakiwa Meru na uongozi ulikubaliana na MCAs kwamba wanapaswa “kutekeleza majukumu yao ya kikatiba”.

“Kama Imanyara anatoa maoni yake kuhusu kugawana nyadhifa hizo ni maoni yake na si msimamo wa chama. Kama chama tunachovutiwa nacho ni uongozi mzuri katika kaunti ya Meru na wala si mizozo,” Bw Ntuchiu, aliyekuwa naibu gavana na Waziri wa Fedha katika utawala wa Kiraitu Murungi aliambia Taifa Leo kwenye mahojiano ya simu.

Maoni yake yalikaririwa na mkurugenzi mkuu wa chama, Bw Haroun Abuana ambaye alisema kuwa DEP haitaki nyadhifa.
Alipotafutwa kutoa maoni, Bw Imanyara alishikilia msimamo wake, akisisitiza kwamba “hatuwezi kwenda kuwinda bila kwanza kukubaliana jinsi ya kugawana nyama.”

“Nataka kujua ni nini kipo ndani yake kwa chama changu. Sitaunga mkono kuondolewa mamlakani kwa gavana Mwangaza ikiwa hatutaweka mezani chama changu kitapata nini. Iwapo watakataa kujadili basi DEP haitaunga mkono kutimuliwa kwa gavana” alisema.

Kinara wa walio wachache, Bw Denis Kiogora alisema hawakutaka wadhifa wowote baada ya kuondolewa madarakani, na kumshutumu Bw Imanyara kwa kumezea mate kiti cha naibu gavana iwapo wangefanikiwa kumtimua Bi Mwangaza, shutuma ambazo katibu mkuu alikanusha.

“Kama DEP hatutaki chochote na kama anataka wadhifa wowote atuambie. Katibu Mkuu anafaa kujua kwamba sisi ni wanachama wa bunge la kaunti na tutafanya shughuli zetu kwa uungwaji mkono au bila uungwaji mkono wa chama.

Kuhusu nyadhifa tutaamua tunachotaka katika Uchaguzi Mkuu wa 2027,” akasema mwakilishi wadi wa Abogeta Magharibi ambaye aliwasilisha hoja ya kwanza ya kuondolewa mashtaka dhidi ya Bi Mwangaza.

  • Tags

You can share this post!

Waislamu wakashifu kitabu chenye mchoro wa Mtume unaotaka...

Mama wa Taifa avalia mavazi ya bei ghali siku ya Utamaduni

T L