• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 9:50 AM
Millicent Omanga atiririkwa na machozi Man U ikicharazwa mabao matatu na Arsenal

Millicent Omanga atiririkwa na machozi Man U ikicharazwa mabao matatu na Arsenal

NA MWANGI MUIRURI
WAZIRI Msaidizi (CAS) mteule wa Idara ya Usalama, Millicent Omanga anaomboleza kichapo ambacho Manchester United ilipokezwa mnamo Jumapili, Septemba  3, 2023 na timu ya Arsenal katika mchuano wa Ligi ya Premier unaoendelea.

Bi Omanga, alikuwa amesafiri London, Uingereza akiwa mwingi wa matumaini Manchester United – Man U ingecharaza Arsenal katika kipute kilichochogaragazwa Uwanjani Emirates.

“Hii nayo lazima ningeona mbashara…Man U hapa ni ushindi,” Omanga aliandika kupitia akaunti yake rasmi ya Facebook.

Alifanya chapisho hilo akiwa katika Uwanja wa Emirates, Jijini London.

Hata hivyo, baada ya timu yake kulimwa mabao matatu kwa moja na Arsenal, CAS huyo hakuwa na budi ila kukiri nyota ya Man U iliwaponyoka.

“Ni mchuano bora ambao Manchester United imecheza msimu huu. Kushindwa kwenye uchungu,” Bi Omanga aliomboleza.

Katika mechi ya Jumapili, mabao ya Martin Ødegaard, Declan Rice na Gabriel Jesus wa Arsenal yalifanikisha kunyamazisha kiherehere cha mashabiki wa Man United.

Vijana hao wa Mikel Arteta wakiwa nyumbani katika uga wa Emirates, walitikisiwa nyavu zao mara moja tu huku wakitoa ndani mara tatu.

Man United walitangulia kwa baa wakidhania kuwa watalewa wakiwa wa kwanza lakini ikawa tembo yao imejaa maji, huku Arsenal wakibugia makali kama moto.

Kifaa Ødegaard katika dakika ya 28 alitikisa nyavu za vijana hao wa Erik Ten Hag, Rice akaongeza moto kwenye kidonda kinachouguza katika dakika ya 96 naye Jesus akafunga jeneza la Man U katika dakika ya 101.

Marcus Rashford alikuwa amezua hali ya taharuki kwa wazito wa Arsenal mnamo dakika ya 27 lakini ikaishia hali ya kuyeyuka kama hewa yabisi.

Ni mechi ambayo Man United ililemewa katika kila safu huku Arsenal ikipiga mikiki 17 dhidi ya 10.

Aidha, mikiki ya Arsenal iliyolenga lango ilikuwa mitano huku Man U ikifaulu miwili pekee.

Huku umiliki wa mpira kwa wanabunduki ukiwa asilimia 55, Man U waliweza tu 45 huku pasi za Arsenal zikiwa 531 dhidi ya 456.

Ulengaji shabaha wa pasi za Arsenal ulikuwa katika kiwango cha asilimia 87, Man U wakiwa kwa asilimia 84.

Arsenal walicheza ngware 8 dhidi ya 7, huku vijana hao wa Arteta wakipata kadi mbili nyekundu dhidi ya tatu za vifaa hao wa Ten Hag.

Wote wakiponyoka kadi nyekundu, Arsenal walijipata wamejenga kibanda kwa wenyewe bila idhini mara 2 huku wapinzani wao wakijipata katika hali hiyo mara moja.

Arsenal walipata kona 12 ishara ya kuwasukuma Man U hadi eneo hatari huku kona za Man U zikiwa mbili tu.

Timu hizo mbili huwa na ushindani sawa na wa United Democratic Alliance (UDA) na Azimio, wote wakibishania ubabe ugani.

Mashabiki wa Man U nchini wamejipata katika dua mbaya ya Seneta maalum Karen Nyamu aliyewaombea msimu mbaya iwezekanavyo.

Katika ligi ya 2022/23, Arsenal ilimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Man City huku Man United wakimaliza katika nafasi ya tatu.

Baada ya kuingia ugani mara nne sasa, Arsenal iko katika nafasi ya tano ikiwa na pointi 10 huku Man United ikiwa ya 11 na pointi 6 katika jedwali ambalo Man City inaongoza kwa pointi 12 baada ya kushinda mechi zake zote.

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Ajabu mume na mke wakubaliana kuchuuza uroda ili wapate mali

Diwani wa UDA ashtakiwa kumteka nyara na kumpiga mwalimu

T L