• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Misongamano inavyotatiza huduma za dharura jijini

Misongamano inavyotatiza huduma za dharura jijini

Na BENSON MATHEKA

JUHUDI za kupunguza misongamano ya magari katikati mwa jiji la Nairobi huwa haziwafurahishi watu wengi hasa wenye magari ya uchukuzi na wanaofanya kazi katikati mwa jiji.

Lakini kwa kampuni na mashirika yanayotoa huduma za dharura jijini kama vile madereva wa ambulensi, zima moto, polisi na kampuni za ulinzi ni baraka kubwa kwao.

Madereva wa ambulansi wanaohudumu jijini wanasema kuwa huwa wanaguswa moyo wanapowaona wagonjwa wanaobebwa katika ambulansi wakipelekwa kupata matibabu maalum wakisononeka katika msongamano wa magari barabarani.

“Ni jambo la kuudhi mno,” asema Bwana Eric Munywoki, anayeendesha ambulansi ya shirika moja jijini.


Bw Eric Oduor, dereva wa ambulensi asema ni mlima kufikisha mgonjwa hospitalini kwa sababu ya msongamano. Picha/ Benson Matheka

Munywoki asema kuwa kwa miaka minane ambayo amekuwa akihudumu jijini ameshuhudia watu wakipoteza maisha yao katika hali ambayo kama sio msongamano wa magari barabarani wangepona.

Anatoa mfano wa wakati ajali inapotokea na wanaitwa ili kuwapeleka wanaonusurika hosptalini.

“Wakati mwingine tunachukua muda mrefu kufika kwenye tukio ili kuwaokoa majeruhi tukipambana kwenye misongamano,” asema na kuongeza kuwa kuna nyakati anapotiririkwa na machozi mgonjwa anapokata roho akiwa amekwama barabarani na matabibu wakimhudumia kwa vifaa haba ndani ya ambulansi.

Dereva huyu anawalaumu madereva jijini kwa kutowapisha watoaji huduma za dharura hata kama ving’ora vinalia.

“Sielewi nia ya waendeshaji magari katika jiji hili. Hawana nidhamu, huwa wanapuuza ving’ora vya magari maalum kama ambulensi na wazima moto,” asema.

Maoni yake yanaungwa na aliyekuwa naibu mkurugenzi wa huduma za zima moto katika baraza la jiji Bw Peter Ngugi anayesema kuwa huduma za wazima moto huvurugwa kabisa na misongomano ya magari.

“Si ajabu kuwaona madereva wametulia tuli huku ving’ora vya magari ya wazima moto vikichana hewa,” asema Ngugi.

Kutokana na kukwama kwao katika misongamano, aeleza Ngugi, wakazi hulaumu idara za kutoa huduma hizi muhimu kwa kuzembea.

“Ieleweke bayana kuwa hakuna wakati idara yetu hukawia tunapopata habari kuwa moto umetokea katika eneo fulani.

Tatizo kubwa ni barabara zetu ambazo zimejaa magari na kutatiza huduma zetu,” asema.

Kutokana na hali hii, hasara kubwa hutokea mali ya mamilioni ya pesa inapoteketea zima moto likiwa limekwama katika msongamano barabarani.

Ngugi anapendekeza kuwa barabara muhimu za jiji zitengewe watoaji huduma za dharura ili wapate fursa ya kutekeleza kazi yao bila kutatizika.

“Sisemi magari yaondolewe kabisa. Ninachopendekeza ni kwamba baadhi ya magari yakatazwe kutumia barabara muhimu ili kurahisisha kazi yetu, ”asema.

Anaunga mkono pendekezo la awali ambapo serikali ilinuia kutenga laini maalum kwa msafara wa Rais, makamu wake na Waziri mkuu.

“Kwa maoni yangu laini iliyokusudiwa kutengewa viongozi hawa inafaa kutengewa magari ya wanaotoa huduma za dharura ili kuboresha huduma jijini, ” asema.

Kulingana na watoaji wa huduma mizunguko iliyo katika barabara kuu inapaswa kuondolewa ili kurahisha usafiri jijini.

Wanasema mingi ya misongamano hutokea kwenye mizunguko hii.

Bw Munywoki aliwaondolea lawama maafisa wa polisi wanaoelekeza magari jijini akisema kuwa huwa wanafanya kazi nzuri .

“Ukweli ni kwamba jiji hili lina magari mengi na mpangilio mbaya wa barabara. Nawashukuru maafisa wa polisi ambao licha ya ongezeko la magari kwenye barabara hizi huwa wanafaulu kuelekeza magari na kupunguza misongamano,” asema.

Hata hivyo anasema baadhi yao huwa hawatilii maanani ving’ora vya magari yao na huendelea kuzuia magari.

“Kuna wanaopuuza ving’ora vya ambulensi na wazima moto na hii haifai. Wanapaswa kufungulia magari ili watoaji wa huduma wafanye kazi na kuokoa mali na maisha,” asema.

Lakini afisa mmoja wa trafiki tuliyeongea naye katika barabara ya uhuru jijini kwa sharti kuwa hatutataja jina lake alisema huenda watu wakawalaumu kwa kutojali magari yanayotoa huduma za dharura jijini kwa kuwa hawaelewi ugumu wa kazi yao.

“Hii ni kazi gumu mno.Watu wanaweza kudhani hatujali wazima moto na magari mengine kama ambulensi kwa sababu hawaielewi,” alisema na kuongeza kuwa kazi yao ni kuongoza na kuelekeza magari tu na sio kujenga barabara.

“Serikali inapaswa kuchukua hatua ili kutafuta suluhisho ya kudumu la msongamano jijini,” asema na kuongeza hilo ni jukumu la serikali ya kaunti na wizara husika katika serikali kuu.

Wengi wa wanaotoa huduma hizo wanasema hatua madhubuti zapaswa kuchukuliwa ili kuondoa kabisa magari katikati mwa jiji na kupunguza kwa kiwango kikubwa magari kwenye barabara muhimu jijini.

“Huwa tunatatizika tunapofanya kazi yetu ya kuhudumia wakazi wa jiji,” asema Bw Vincent Kea, mfanyakazi wa kampuni moja ya ulinzi anayehudumu katikati mwa jiji.

Bw Vincent Oduor Kea, dereva wa kampuni ya ulinzi alalamika misongamano hutatiza kazi yao. Picha/ Benson Matheka

Kea aeleza kuwa wafanya kazi wa kampuni za ulinzi hupata wakati mgumu wanapotakiwa kuhudumia mteja wao linapotokea jambo la dharura.

“Ni kama kupasua mwamba kupata maji kujaribu kupenya msongamano wa magari katika barabara za Nairobi ukielekea kumuokoa mteja anapotoa kilio cha dharura,” asema Kea ambaye amefanya kazi hii kwa miaka 12.

Anasema huwa ni vigumu kuwaauni wateja wao hasa walio katikati mwa jiji kwa kuwa wanachelewa wakijaribu kupita katika misongamano ya magari.

“Mara nyingi huwa tunachelewa katika misongamano ya magari tunapoarifiwa kuwa mteja anahitaji huduma zetu,” asema.

You can share this post!

Mikutano ya uhamasisho BBI iwe na utaratibu mzuri –...

Zogo lanukia Ruto akitarajiwa katika mkutano wa BBI Meru

adminleo