• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Mpasuko Azimio kuhusu ‘mchujo’

Mpasuko Azimio kuhusu ‘mchujo’

NA LEONARD ONYANGO

MVUTANO umeibuka ndani ya muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya kutokana na pendekezo la kuwatema baadhi ya wawaniaji wa vyama tanzu wasio na umaarufu.

Baraza Kuu la Azimio la Umoja, mnamo Ijumaa, liliidhinisha mpango wa kuwataka wawaniaji ‘dhaifu’ wajiondoe ili kuepuka kugawanya kura.

Waziri wa Ulinzi, Bw Eugene Wamalwa jana alionekana kupuuzilia mbali uamuzi huo huku akisema kuwa wawaniaji wote wa chama chake cha DAP-K watashiriki katika uchaguzi wa Agosti 9.

Bw Wamalwa aliyekuwa akizungumza katika eneobunge la Teso Kusini, Busia katika hafla ambapo mwaniaji wa Uwakilishi wa Wanawake, Evalyne Omasaja alitawazwa na wazee, aliwataka wawaniaji wa DAP- K kutokuwa na hofu ya kutemwa.

Bi Omasaja anamenyana na Bi Catherine Omanyo (ODM), Bi Mary Makokha (MDG) na Bi Susan Auma Mang’eni wa UDA inayoongozwa na Naibu wa Rais William Ruto. ODM, MDG na DAP-K ni miongoni mwa vyama 26 vilivyo ndani ya muungano wa Azimio.

Ripoti za utafiti wa kura za maoni za hivi karibuni zinaonyesha kuwa ushindani mkali unatarajiwa baina ya Bi Omanyo na Bi Makokha. Wawaniaji hao huenda wakagawanya kura na kutoa mwanya kwa mwaniaji wa UDA kuibuka na ushindi.

Lakini Bw Wamalwa alimtaka Bi Omasaja kutokuwa na wasiwasi huku akisema hakuna mwaniaji wa DAP-K atakayetolewa kwenye kinyang’anyiro.

“Kila mwaniaji aliyeidhinishwa na DAP-K na IEBC (Tume ya Uchaguzi) atashiriki uchaguzi wa Agosti 9. Hakuna mtu atakayelazimishwa kujiondoa au kufinywa na Azimio,” akasema Bw Wamalwa.

Kiongozi wa UDP, Bw Cyrus Jirongo pia amepuuzilia mbali uamuzi wa Baraza Kuu la Azimio huku akisema kuwa chama chake hakitaondoa wawaniaji wake.

“Mwaniaji wa urais wa Azimio, Bw Raila Odinga ana chama chake (ODM), mimi pia nina chama changu (UDP). Mtu asiniambie kutosimamisha wawaniaji. Ninajua hiyo ni njama ya vigogo wa Azimio kuua vyama vidogo,” akasema Bw Jirongo alipokuwa akizindua kampeni yake ya ugavana mjini Kakamega.

Bw Jirongo anamenyana na Fernandes Barasa wa ODM na Seneta Cleophas Malala wa UDA.

Bw Odinga alipokuwa akifanya kampeni katika Kaunti ya Kakamega mnamo Machi aliidhinisha Bw Barasa kuwa mrithi wa Gavana Wycklife Oparanya.

Mwaniaji mwenza wa urais wa Azimio, Bi Martha Karua, hata hivyo, ameshikilia kuwa wawaniaji wa vyama tanzu vya muungano huo wasio na umaarufu watazuiliwa kuwania. Kulingana na Bi Karua, muungano huo utafanya kura za maoni kusaka wawaniaji maarufu watakaopeperusha bendera ya Azimio na kutema wengine.

“Azimio tukiwa na wawaniaji watatu, kwa mfano, na wapinzani wetu (wa Kenya Kwanza) wasimamishe mwaniaji mmoja, tutabwagwa,” akasema Bi Karua alipokuwa akihutubia jamii ya Wakikuyu katika eneo la Gilgil, Nakuru, Jumamosi.

Muungano wa Azimio umeanza kushawishi baadhi ya wawaniaji kujiondoa kwa kuwapa ahadi ya kuteuliwa serikalini endapo Bw Odinga atashinda urais.

Muungano huo umetishia kuanzisha kampeni kali dhidi ya wawaniaji watakaokataa kujiondoa kupisha wawaniaji wa Azimio walio na umaarufu.

Bi Karua amewasihi wawaniaji watakaotemwa kutozua taharuki ndani ya Azimio na badala yake waunge mkono watakaopewa tiketi ya muungano huo.

Mikutano ya kampeni za Azimio katika eneo la Kaskazini Mashariki imekumbwa na vurugu huku wawaniaji mbalimbali wakishindana kudhihirisha umaarufu wao kwa kuleta wafuasi wao.

Jumamosi asubuhi, wafuasi wa mwaniaji wa ubunge wa Mandera Mashariki Omar Maalim wa UDM walikabiliana na wale wa mpinzani wake Hussein Weytan wa ODM katika uwanja wa Mandera kabla ya Bw Odinga na Bi Karua kuwasili.

Baadaye, wawaniaji wa ODM walifanya mkutano na Bw Odinga pamoja uwanjani hapo na mkutano mwingine na wawaniaji wa UDM ukafanyiwa uwanjani Takaba, Mandera Magharibi.

Alhamisi, maafisa wa polisi waliamua kutumia vitoa machozi kutawanya umati baada ya wafuasi wa Gavana Mohamud Ali na Waziri wa Fedha, Ukur Yattani kukabiliana mbele ya Bw Odinga katika Kaunti ya Marsabit.

Viongozi wa Azimio pia watakuwa na kibarua kigumu kuchuja mmoja kati ya Gavana Joseph Ole Lenku (ODM) na Gavana wa zamani David ole Nkedianye (Jubilee) ambao wote wanawania ugavana.

Hali kama hiyo itashuhudiwa katika kaunti za Kisii na Nyamira.

Katika Kaunti ya Nyeri, Azimio ina wawaniaji wawili; Priscilla Nyokabi (Jubilee) na mbunge wa zamani wa Mukurwe-ini, Bw Kabando Kabando (Narc-K).

  • Tags

You can share this post!

Kocha Wayne Rooney ataka vinara wa Derby County wamwachishe...

KRA yazindua mfumo wa kuunganisha risiti za biashara na...

T L