• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
Msajili wa Vyama akaangwa kwa kuzembea kusafisha orodha ya wanachama

Msajili wa Vyama akaangwa kwa kuzembea kusafisha orodha ya wanachama

Na CHARLES WASONGA

SUALA la Wakenya kujipata wamesajiliwa katika vyama vya kisiasa kinyume cha matakwa yao Alhamisi liliendelea kumzonga Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu alipofika mbele ya wabunge.

Hii ni baada ya Mbunge wa Dagoretti John Kiarie kulalamika kuwa juzi aligundua kuwa bado ameorodheshwa kama mwanachama wa ODM ilhali alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha Jubilee katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Bw Kiarie alisema aligundua hitilafu hiyo hivi majuzi alipokuwa akijaribu kujiuzulu kutoka Jubilee na kujiunga na chama cha United Democratic (UDA) kupitia nambari ya USSD, *509#.

“Nilijaribu kujiuzulu kwa kutumia nambari ya *509# lakini nikagundua kuwa kwanza mimi sio mwanachama wa chama Jubilee ambacho nataka kuhama ili nikiunge na Jubilee.,” akasema.

Bw Kiarie aliongeza kuwa sasa atalazimika kujiuzulu kwa njia ya kawaida kutoka vyama hivyo viwili (ODM na Jubilee) kabla ya kusajiliwa rasmi kuwa mwanachama wa UDA.

Mbunge huyo ni miongoni mwa wanachama wa Jubilee ambao wamekaidi chama hicho tawala na kuamua kujihusisha na chama cha UDA, kinachoshirikishwa na Naibu Rais William Ruto.

Kulingana na sheria mpya ya vyama vya kisiasa iliyoanza kutekelezwa mnamo Februari 11, 2022, orodha sahihi ya wanachama wa vyama vya kisiasa ndio itatumiwa na Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Kulingana na sheria hiyo wale watakaoshiriki katika kura za mchujo kama wasakaji tiketi za kuwania viti mbalimbali na watakaowapigia kura wawaniaji hao sharti wawe wanachama rasmi wa vyama husika.

Kulingana na mwongozo uliotoelwa na  Bi Nderitu vyama vya kisiasa vinapaswa kuwasilisha orodha sahihi ya wanachama wake kwa afisi yake kufikia Machi 26, 2022. Baadaye afisi hiyo itawasilisha sajili hiyo kwa IEBC baada ya kuipiga msasa na kuthibitisha kuwa ni sahihi.

Bi Nderitu ambaye alikuwa amefika mbele ya kamati ya bunge kuhusu haki na masuala ya kikatiba (JLAC) katika majengo ya bunge, Nairobi, alijitetea afisi yake akisema hitilafu hiyo ilitokea chini ya sheria ya zamani.

“Shida hii ambayo ilimkubwa Mheshimiwa Kiarie imewakumba Wakenya wengi. Lakini ningependa kuhakikishia kamati hii kwamba tunapambana nayo licha ya kwamba chanzo chake ni udhaifu wa sheria ya zamani,” akawaambia wanachama wa kamati hiyo wakiongozwa na mwenyekiti wao Muturi Kigano (Mbunge wa Kangema).

Bi Nderitu alikuwa amefika alifika mbele ya kamati hiyo kuelezea jinsi afisi yake inavyotekeleza sheria hiyo mpya iliyopitishwa Januari 15.

Aliahidi kutatua tatizo hilo na matatizo hayo ili kuowaondolea Wakenya na wagombeaji usumbufu wakati wa kura za mchujo zinazoanza Aprili, 2022.

Tangu mwaka jana, Wakenya wamekuwa wakilalamika kuwa wanasajiliwa katika vyama ambavyo hawaamini sera yavyo na bila hiari yao.

  • Tags

You can share this post!

Afisa wa KRA afikishwa kortini kwa penzi la mauti

WANDERI KAMAU: Uhuru hafai kutumia lugha ya mama katika...

T L