• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:55 AM
Mtambo unaochemsha na kuhifadhi maziwa yakisubiri kupata soko

Mtambo unaochemsha na kuhifadhi maziwa yakisubiri kupata soko

Na RICHARD MAOSI

WAKULIMA wanaokamua maziwa kutoka kwa nafaka aina ya soya, wafugaji wa ng’ombe na mbuzi wa maziwa wanaendelea kupata hasara kutokana na mifumo duni inayotumika kuhifadhi bidhaa yenyewe.

Hata hivyo, teknolojia ya kisasa ya pasteurization (mtambo wa kuchemsha maziwa kwa nyuzi joto 99.9 ) umekuja na jawabu mwafaka , kwanza kwa kuhakikisha virutubishi muhimu kama vile vitamini, protini na madini ya calcium yanasalia ndani ya maziwa.

“Ni mtambo ambao unaweza kununuliwa na wakulima wadogo mashinani wanaolenga kuanzisha muungano wa kuuza maziwa mashinani,”anasema Dorothy Barusi mshauri wa kilimo-bishara.

Anasema kuwekeza kwenye mitambo iliyoboreshwa kiteknolojia ni mpango wa kukuza kilimo miongoni mwa wakulima wasiokuwa na mbinu za kuhifadhi mazao ambayo badaye huuzwa kwa bei ya chini.

Alieleza kuwa utunzaji, uhifadhi na usafirishaji wa maziwa ni vipimo vya kimsingi ambavyo wahudumu wa kuyapokea na kukusanya maziwa wanafaa kuelewa.

Anasema hiki ni kifaa cha chuma kilichoundwa kwa alumini, ambacho hakiwezi kupata kutu na huwa ni rahisi kusafisha na kuua vidudu, kinyume na matumizi ya vyombo vya plastiki ambavyo vinaweza kuweka harufu kwenye maziwa.

Isitoshe ni mtambo ambao unaweza kuangamiza vimelea vya bakteria na fangasi, vinavyoweza kupatikana ndani ya maziwa, hii ni kwa sababu maziwa yanayokamuliwa huwa na virutubishi vingi ambavyo ndio chanzo cha mazingira yapendwayo na vimelea kusambaa haraka.

Ikumbukwe kuwa uchuuzi wa maziwa rejereja mbayo hayajakaguliwa vilivyo umekuwa ukiangaziwa kwa kusababisha mkurupuko wa maradhi kama vile salmonella.

Ni mtambo ambao unaweza kuchemsha takriban lita 1000 za maziwa kwa kipindi cha saa moja na kumpunguzia mkulima gharama ya kuyahifadhi hususan msimu wa joto.

Anasema mchakato wa kufanya kazi huwa ni rahisi ikizingatiwa kuwa katika hatua ya kwanza maziwa huingizwa ndani ya tanki maalum yangali baridi, ambapo huanza kuchemshwa taratibu kwa joto la kadri.

Hatimaye huelekezwa baina ya paipu ili kutoa fursa kwa vipimo joto kubainisha ikiwa kiwango sahihi cha joto kimefikiwa, kwa upande mmoja wa aina hii ya tanki huwa ni maziwa ambayo yamechemshwa vilivyo pasipo na vimelea huku sehemu ya pili ikiwa na maziwa freshi yanayoingia ndani ya tanki.

Maziwa hutokea katika aina maalum ya paipu ambazo husaidia kuyapoza na hatimaye kupakiwa ndani ya vyombo vya mabati vilivyosafishwa vyema yakisubiri kusafirishwa sokoni.

Aidha, Akilimali ilimtembelea Sarah Wamboi kutoka eneo la Gatundu, Kiambu ambapo anasema kuwa huu ni mtambo ambao unahakikisha maziwa ni salama kwa binadamu.

Anasema wakulima wanaelewa hasara ambayo wanaweza kukumbana nayo endapo maziwa yao hayatafika sokoni kwa wakati ufaao.

“Ni mtambo ambao unasaidia kuzuia kuharibika kwa maziwa na kuongeza faida kwa wafanyabiashara,”akasema.

Wamboi hukamua maziwa kutoka kwa nafaka za soya na amekuwa akitengeneza maziwa , ambapo anaungama kuwa kipato chake ni kizuri kwa sababu bidhaa yake inaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu bila kuharibika.

Yeye huuza lita moja ya maziwa yanayotokana na soya kwa Sh350, wateja wake wengi wakiwa ni wakazi wa Kiambu, Nairobi na Nakuru, kwani huwa amewahakikishia wateja wake usafi wa hali ya juu.

Uvumbuzi unaonyesha kuwa maziwa ambayo yamechemshwa ndani ya kifaa yanaweza kunyweshwa ndama badala ya wao kuendelea kunyonya, kutoka kwa chuchu za mama zao.

Wala mkulima hana haja ya kuhofia kwamba huenda ndama wake wakakabiliwa na maradhi, jambo ambalo vilevile litapunguza gharama ya kuwatibu mifugo.

Hii itatoa fursa kwa wakulima kuendelea kukama mifugo wake, na kumwongezea mkulima kipato.

You can share this post!

Nafasi finyu mjini lakini ufugaji mbuzi umenawiri si haba

Mwanamke ashukiwa kuwa gaidi

T L