• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Mwanamitindo chipukizi kuwakilisha Kenya katika mashindano ya Ulaya

Mwanamitindo chipukizi kuwakilisha Kenya katika mashindano ya Ulaya

NA RICHARD MAOSI

KAMA wanavyosema safari huanza kwa hatua moja, ndiyo hali halisi kwa binti mdogo Quinn Anna Njoki ambaye anatamba katika tasnia ya urembo.

Taifa Leo , ilipomtembelea nyumbani kwao mtaa wa Racecourse Nakuru, tulimkuta mwanamitindo huyu chipukizi, akijipiga msasa kupitia aina mbalimbali ya miondoko.

Quinn atawakilisha Kenya kwenye mashindano ya Little Miss Universe yatayofanyika Batumi bara Uropa 2021 , analenga kuwashinda wapinzani wake, na kutwaa nishani ya dhahabu.

Ingawa anahitaji kitita cha takriban 600,000 kufanikisha safari yake ana matumaini makubwa kuwa mashabiki zake, wahisani na hata Rais Uhuru Kenyatta watamsaidia kutimiza azma yake.

Kulingana naye alianza kujifunza uanamitindo akiwa na miaka minne nyumbani kwao , na hatimaye akaboresha tajriba mamake alipomlipia ada ya kujifunza uanamitindo kwenye taasisi moja mjini Nakuru.

Hapo alijifundisha kutembea kwa madaha akitumia aina mbalimbali ya miziki ya kizazi kipya,, na nyota yake ilianza kung’aa alipoanza kushiriki kwenye majukwaa ya urembo ndani na nje ya kaunti ya Nakuru.

Kipaji chake kilimzolea sifa tele akaanza kuwaniwa na mashirika kadhaa ya urembo, lakini kutokana na umri wake mdogo hangeweza kuingia kwenye mikataba ya kudumu, ikizingatiwa kuwa bado alikuwa ni mwanafunzi wa gredi ya nne.

Alitumia muda wake mwingi kufanya mazoezi na wakati huo kuzingatia masomo yake, ikizingatiwa kuwa alichukua muda mfupi kubobea.

Kuanzia 2019 kabla ya mkurupuko wa covid-19 humu nchini Quinn amekuwa akishiriki kwenye mashindano mbalimbali katika ukanda wa Bonde la Ufa kwa mfano Little Miss Nakuru ambapo amekuwa akifanya vyema na kuwabwaga wenzake.

Quinn anasema kuwa motisha yake kubwa ni kutokana na mashabiki pamoja na wazazi wake ambao wamekuwa wakimpatia msukumo wa kujibidiisha kila siku.

Mwanzoni wa mwaka wa 2021, Quinn aliteuliwa kuwakilisha Kenya kwenye mashindano ya urembo na uanamitindo ambayo yatafanyika Batumi Georgia Uropa kuanzia Juni 2021.

“Mashindano hayo ambayo yatashirikisha watoto wengine wengi kutoka kote ulimwenguni yamenifanya kuamini kuwa kipaji kinaweza mfikisha mtu mbali,”akasema.

Kufikia sasa Quinn anatumia mtandao wa kijamii kama fesibuku,watsap na twitter kutengeneza uga wa mashabiki ambao wanafuatilia kazi zake huku akiwahimiza waendelee kumpatia usaidizi wa ushauri au fedha ili kufanikisha safari yake.

Anaamini kuwa ndoto yake itakuja kung’aa kwenye kiwango cha kimataifa haitazima muradi ataweka Mungu kwanza na kuzingatia mambo yote muhimu ambayo mwalimu wake amekuwa akimfundisha.

Isitoshe Quinn anawashauri wazazi kuwapatia watoto wao muda wa kufuata ndoto zao, pamoja na kuwaelekeza kwa njia za maadili mema.

  • Tags

You can share this post!

Mchuuzi wa ndizi taabani kwa kupatikana na Sh900,000 ndani...

BBI: Reggae yazimwa kwa mara ya tatu