• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
Mwatate FC yajipanga kupanda ngazi ligi kuu ya FKF licha ya kuaibishwa na Fortune

Mwatate FC yajipanga kupanda ngazi ligi kuu ya FKF licha ya kuaibishwa na Fortune

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

MBALI na Mwatate United FC ya Kaunti ya Taita Taveta kushindwa kwa bao 1-0 na Fortune Sacco FC katika mechi yao ya ufunguzi ya Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL), imepania kuhakikisha imepanda ngazi hadi Ligi Kuu ya FKF msimu ujao.

Kulingana na Meneja wa timu hiyo, Christopher Nyamao, kushindwa huko kumewafanya kupata muda mzuri wa kujirekebisha kwani ligi ndio mwanzo imeanza.

“Imekuwa si vibaya kushindwa huko kwani tutajirekebisha na kuhakikisha tunashinda mechi zetu zijazo,” akasema Nyamao.

Huu ni msimu wa pili kwa Mwatate kushiriki kwenye ligi hiyo na Nyamao amesema wamepania kuhakikisha wanapanda ngazi hadi ligi kuu.

“Ninaamini tunaweza kufanya vizuri kwenye mechi zetu zijazo,” akasema meneja huyo.

Nyamao amesema wanasoka wake walionyesha mchezo mzuri wa hali ya juu ambao umempa matumaini makubwa ya mwaka huu kuwa na uwezo wa kushinda taji la NSL na kupanda hadi ligi kuu msimu ujao.

“Kwa jinsi vijana wangu walivyocheza mchezo wa hali ya juu, sina wasiwasi tutafanya vizuri msimu huu na lengo letu kubwa ni kuhakikisha tunapata mojawapo ya nafasi za kupanda ngazi hadi ligi kuu,” akasema.

Hata hivyo, Nyamao amesema hakuridhika jinsi refarii alivyochezesha mchezo huo kwani anadai maamuzi yake yalikuwa ya wazi ya kupendelea wapinzani wao waliokuwa wakicheza uwanja wa nyumbani.

“Sisi hatupendi kulalamika lakini tungelitaka wasimamizi wa ligi waangalie mapema juu ya waamuzi ambao huchukua hatua za kupendelea timu za nyumbani kwani kufanya hivyo, kunaweza kuua mchezo huu unaopendwa na Wakenya wengi,” akasema Nyamao.

Alitoa wito kwa waamuzi wawe wenye kutumia haki na kufuata sheria za uchezeshaji mpira ili hali ya soka ipate kuinuka nchini.

“Lakini kupendelea na kuiadhibu timu isiyofanya makosa, kunaweza kuathiri na kuumiza maendeleo ya mchezo huo,” akasema.

You can share this post!

Kaburi la Mekatilili sasa kugeuzwa ‘chuo’ cha utamaduni

TAHARIRI: Tushabihiane na hadhi yetu katika riadha

T L