• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Mwatate, Bomet watoka sare 2-2

Mwatate, Bomet watoka sare 2-2

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

BAO la penalti lilofungwa na Marven Akhouya dakika ya majeruhi liliisaidia Mwatate United kugawanya pointi na AP Bomet FC kwenye mechi ya National Super League (NSL) iliyotandazwa katika uwanja wa Dawson Mwanyumba mjini Wundanyi.

Mechi hiyo iliyochezwa kabla ya pambano la Ligi Kuu ya FKF kati ya Sofapaka na AFC Leopards, timu hizo za Mwatate na Bomet zilikuwa zimefungana bao 1-1 hadi wakati wa mapumziko.

Bomet ilichukua uongozi kunako dakika ya nne kupitia kwa bao la penalti lilofungwa na Swaleh Abdalla lakini Mwatate ilipigana na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha lilotingwa nyavuni na Cornelius Juma pia kupitia mkwaju wa penalti kunako dakika ya 25.

Katika kipindi cha pili, Bomet ilifanikiwa kuchukua tena uongozi wakati Felix Oluoch alipoifungia kunako dakika ya 70 lakini Mwatate haikukubali kuondoka bila ya pointi wakati Akhouya alipofunga bao la kusawazisha dakika ya pili ya muda wa ziada.

Kocha wa Mwatate United FC, Andrew Kanuli aliwapongeza wachezaji wake kwa kuonyesha ujasiri wakati walipofungwa bao la pili hadi wakaweza kukomboa na kuhakikisha wamegawana pointi moja moja.

“Nina furaha sana kwa jinsi vijana wangu walivyopambana viulivyo hadi kupata bao la kusawazisha katika muda wa majeruhi. Ninaamini tutafanya vizuri zaidi mechi ijayo,” akasema Kanuli.

Naye kocha wa Bomet FC, Benedict Wanjala alilalamikia uamuzi wa refarii wa kuwapa wapinzani penalti ambayo alisema haikuwa ya haki. “Tulistahili kuondoka na alama zote tatu lakini uamuzi wa kuwapa Mwatate penalti ulikuwa wa kutuonea,” akalalama Wanjala.

Mwatate United ambayo inashiriki katika ligi hiyo kwa mara ya kwanza ndiyo inayofanya vizuri kati ya timu nyingine mbili za Pwani, Modern Coast Rangers na Coast Stima ambazo zinakabiliwa na matatizo ya udhamini.

You can share this post!

Mutua akubali Ruto ni maarufu Mlima Kenya

Walevi Gatundu waasi pombe kujishughulisha na kazi za...