• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Mwendwa aachiliwa kwa dhamana ya Sh4Milioni pesa taslimu

Mwendwa aachiliwa kwa dhamana ya Sh4Milioni pesa taslimu

Na RICHARD MUNGUTI

Rais wa Shirikisho la Kandanda Nchini (FKF), Nick Mwendwa amepata afueni baada ya kuachiliwa kwa dhamana ya Sh4 milioni pesa taslimu.

Mwendwa aliachiliwa baada ya kuzuiliwa kwa siku tatu. Mwendwa aliondoka seli ya mahakama ya Milimani mwendo wa saa moja jioni baada ya kulipa dhamana hiyo ya Sh4milioni pesa tasilimu. Punde tu baada ya kutoka alipokewa na Rais wa Chama cha mawakili nchini Nelson Havi naibu wake Bi Caroline Kamende, wakili mwenye tajriba ya juu Prof Tom Ojienda na Charles Njenga.

Akimwachilia kwa dhamana, hakimu mwandamizi Wandia Nyamu alimwekea masharti makali. Bi Nyamu alimwamuru Mwendwa asiende karibu na afisi za FKF zilizoko Kandanda House, Kasarani. Pia aliamriwa asihutubie wanahabari wala kuzungumza na wafanyakazi wa FKF.

Pia aliagizwa asiwavuruge wafanyakazi wa FKF. Mbali na hayo aliagizwa asiwahutubie wanahabari na wala asijihusishe na shughuli zozote za FKF. “Usijihusishe na shughuli zozote za FKF. Hata usihudhurie mchezo kati ya Harambee Stars na Rwanda katika uwanja wa Nyayo,” Mwendwa aliagizwa.

Mawakili walioongozwa na rais wa zamani wa chama cha wanasheria nchini (LSK) Eric Mutua, Dkt John Khaminwa, Prof Ojienda, Mutula Kilonzo Jnr, Charles Njenga na Sylvia Matasi waliomba mahakama imwachilie rais huyo wa shirikisho la kandanda nchini kwa dhamana.

Bw Mutua, Prof Ojienda, Kilonzo Jnr na Dkt Khaminwa walieleza hakimu kuwa Serikali na Polisi walieneza habari sisizo na msingi kwamba “Mwendwa amefuja zaidi ya Sh513milioni ilhali ushahidi waliowasilisha mahakamani ni Sh38milioni.” Bw Mutua alieleza mahakama kwamba uvumi huu wa polisi na msajili wa FKF hauna msingi wowote.

“Serikali haihusiki kamwe na masuala ya kabumbu. FKF inasimamiwa na watu binafsi kwa ushirikiano wa Chama cha Soka barani Afrika (CAF) na Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa),” alisema Bw Mutua. Mahakama ilielezwa kuwa kamati iliyoteuliwa na Waziri wa Michezo Amina Mohamed haitambuliwi na Fifa na Caf.

Bw Mutua alieleza mahakama Fifa iliwasilisha barua Novemba 14, 2021, inayotisha kupiga marufuku Kenya kushiriki katika michuano ya kimataifa endapo”haitakoma kuingilia masuala ya FKF.” Mutua aliambia hakimu polisi na maafisa wakuu Serikalini walipotosha umma kwa madai hayo yasiyo na msingi.

Mahakama iliambiwa masuala ya kandanda nchini hayahusiani na utenda kazi wa Serikali kwa vile yanasimamiwa na mashirika ya CAF na Fifa. Mutua aliwasisilisha Kortini barua kutoka kwa Fifa ya Novemba 14 ikitisha kuipiga marufuku Kenya kushiriki katika mechi za kimatifa iwapo Serikali haitakoma kuingilia masuala ya soka nchini.

“Kamati ya Ringera haitambuliwi na Fifa, na hata hawawezi kutekeleza majukumu ya FKF chini ya Mwendwa,” alisema Khaminwa. Khaminwa aliongeza masuala ya kandanda yanasimamiwa na watu binafsi kama Mwendwa na wala sio Serikali. Ojienda aliambia Korti kwamba iwapo Serikali itaendelea kuvuruga utaratibu wa FKF, vilabu na wachezaji wa kandanda watateseka kwa kiasi kikubwa na wafanyakazi wa FKF hawatapata mishahara na marupurupu yao kwa vile Fifa na mashirika mengine yatakoma kufadhili shughuli za kandanda.

Bi Nyamu alitoa agizo hilo na kuvuruga ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma nchini(DPP) Noordin Haji aliyeomba mahakama imzuilie Bw Mwendwa kwa siku 14 kuwezesha polisi kukamilisha uchunguzi. Mahakama ilielezwa kuna hati za FKF ambazo polisi wanataka kusoma na ziko na Mwendwa.

Kiongozi wa mashtaka Bi Everlyne Onunga aliomba mahakama imzuilie Mwendwa ili polisi wakamilishe. Onunga alisema Mwendwa atavuruga mashahidi akiachiliwa kwa dhamana. Hakimu alimwachilia kwa dhamana na kueleza atatoa sababu zaidi Novemba 17,2021.

You can share this post!

Hatimaye Stars, Firat waonja ushindi

Polisi walioua bila kukusudia jela miaka 48

T L