• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
Nacada yalilia kituo cha kurekebisha tabia

Nacada yalilia kituo cha kurekebisha tabia

Na WACHIRA MWANGI

MAMLAKA ya Kupambana na Pombe na Matumizi ya Dawa za Kulevya (NACADA), imetaja kucheleshwa kwa uhamisho wa kituo cha Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) kama sababu kuu ya kutokamilishwa kwa ujenzi wa kituo kikuu cha kurekebisha tabia miongoni mwa watumiaji wa dawa za kulevya cha Miritini, Mombasa.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Nacada , Bw Victor Okioma wikendi alieleza Kamati ya Bunge kuhusu Usalama na Utawala kuwa kumekuwa na changamoto za kuhamisha kituo cha NYS ambacho kina maafisa 200 wa NYS. Hii ni licha ya Rais Uhuru Kenyatta kuamuru kituo hicho kihamishwe miaka sita iliyopita.

Mnamo 2015, akiwa katika kikao na viongozi wa Pwani, Rais Kenyatta aliamrisha kituo hicho cha NYS cha Miritini kibadilishwe ili kuwasaidia vijana waliotekwa na dawa za kulevya.

Wakati huo, Rais Kenyatta alimtaka Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa na kamanda wa eneo hilo Robert Kitur wawasilishe mpango unaotoa mwelekeo kuhusu njia ya kupambana na kukithiri kwa matumizi ya dawa za kulevya.

“Kutokana na mkutano huo, Rais alisema kuwa kituo cha NYS kirekebishwe ili kiwe kituo cha kuwapa nasaha na kurekebisha tabia kwa wenye uraibu wa dawa za kulevya. Hakuna hatua kubwa iliyopigwa ila tunaendelea kujikaza,” akasema Bw Okioma.

Alisema kuwa kuelekea 2019, Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i alipata ardhi mbadala ya kuhamishiwa kituo cha NYS ila tangu wakati huo, uhamisho wowote haujafanyika.

Aidha Bw Okioma alisema kuwa kontena 100 ambazo zilikuwa zikitoa huduma za kliniki zilikuwa kikwazo cha kujengwa au kuimarishwa kwa kituo hicho cha urekebishaji wa tabia.

“Kutoka Februari 2020 tangu kitengo cha kituo hicho cha kuwahudumia wagonjwa kisha waruhusiwe kwenda nyumbani kizinduliwe, watu 30 ambao walikuwa wamelemewa na matumizi ya dawa za kulevya wamerekebishwa tabia. Kwa sasa kituo hicho kina watu 24 ambao wanaendelea kurekebishwa tabia,” akafafanua.

“Tumekuwa tukishirikiana na idara ya serikali kuhusu ukarabati wa miundo msingi ambapo mpango wa Sh1.2 bilioni unatekelezwa,” akaongeza huku akisema kuwa Kenya ina watu 18,000 ambao wana uraibu wa kutumia dawa za kulevya.

Baada ya kukamilishwa kwa ujenzi wake, kituo hicho kitawahudumia waraibu wa dawa za kulevya 200 kwa wakati moja huku wakilenga hasa wale ambao wametelekezwa na jamii zao kutokana na uraibu mkubwa wa dawa za kulevya.

Kamati hiyo inayoongozwa na mbunge wa Limuru, Bw Peter Mwathi ilisema walikuwa Mombasa kutathmini mipango ambayo imekuwa ikiendeshwa na Nacada pamoja na ujenzi wa kituo hicho, kuwahudumia waraibu wa dawa za kulevya.

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali isilazimishe walimu kusoma tena

Fimbo ya maaskofu yawaumiza