• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
Nairobi Expressway kutatiza usafiri hadi 2022

Nairobi Expressway kutatiza usafiri hadi 2022

Na HILARY KIMUYU

WAKENYA watalazimika kuvumilia msongamano wa magari kwa mwaka mmoja, barabara ya Nairobi Expressway inapoendelea kujengwa.

Waziri wa uchukuzi James Macharia amesema kwamba ikikamilika kujengwa, barabara hiyo inayotarajiwa kuwa ya kuvutia zaidi ukanda wa Mashariki, Kati na Upembe wa Afrika, itapunguza muda wa kusafiri kutoka Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa JKIA na kituo cha garimoshi cha Syokimau hadi katikati na maeneo mengine ya jiji.

Bw Macharia alisema barabara hiyo inatarajiwa kufunguliwa Aprili mwaka ujao.

Akizungumza Ijumaa baada ya kukagua ujenzi wa barabara hiyo katika makutano ya barabara za James Gichuru na Rironi Highway, Bw Macharia aliwahimiza wenye magari na wasafiri kuvumilia akisema wanachoshuhudia kwa sasa ni uchungu wa muda mfupi.

“Kwa wakati huu, ninajua watu wanatatizika sana kwa kutumia muda mrefu kwenye msongamano lakini sababu ya kujenga Nairobi Expressway ni kutatua shida ya msongamano. Kama hakungekuwa na msongamano wa magari, hakungekuwa na sababu ya kujenga barabara hiyo. Uchungu tunaoshuhudia sasa ni uchungu wa muda mfupi,” alisema.

Watu wanaotumia barabara za Mombasa na Uhuru Highway na wale wanaopitia barabara ya Waiyaki ndio walioathiriwa zaidi.

Bw Macharia alisema kwamba japo watu wanapata hasara kwa kukwama kwenye msongamano wa magari kwa muda mrefu, hali ilikuwa sawa na hiyo hata kabla ya ujenzi wa barabara hiyo kuanza na “hasara hizi ndizo tunazotaka kuzuia”.

Kuna viwanda vingi kwenye barabara ya Mombasa na ndiyo hutumiwa kufika eneo la viwandani ambako kuna makampuni makubwa ya kutengeneza na kusafirisha bidhaa.

Ujenzi wa barabara hiyo unatekelezwa na kampuni ya China na unaendelea vyema.

You can share this post!

ODM yakana Oparanya aelekea kwa Ruto

RAILA AMTATIZA UHURU AKILI