• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
NASAHA: Chukua hatua kuimarisha kumbukumbu yako unapojiandaa kwa mtihani

NASAHA: Chukua hatua kuimarisha kumbukumbu yako unapojiandaa kwa mtihani

Na HENRY MOKUA

NAAMINI unazidi kujiandaa kukabiliana na mtihani wako wa mwisho wa muhula au wa kitaifa ikiwa wewe ni mtahiniwa wa kitaifa.

Umezidi kujifunza mengi unayotegemea yakufae hasa wakati wa mtihani.

Licha ya tamaa yako ya kuyakumbuka uliyojifunza, huenda unayasahau punde baadaye pasi na kutarajia…ndiposa nimedhamiria tuangazie namna ya kukuza kumbukumbu za maarifa tunayozidi kuyapata. Ilivyo ada ya kufanikisha mradi wowote wa mno, kuimarisha kumbukumbu kunahitaji kujitolea na wakati mwingine kujihini. Angazia mapendekezo yafuatayo ya kuiimarisha kumbukumbu yako.

Fanya mazoezi ya mwili. Japo mazoezi ya kifikra huchangia makuzi ya akili, mazoezi ya mwili yana nafasi muhimu aidha kwani hushughulisha viungo vingine vya mwili na akili kwa wakati mmoja. Mazoezi ya mwili pia huongeza kiwango cha oksijeni akilini ili kupunguza uwezekano wa kukumbwa na usahaulifu.

Mazoezi yanayohusisha mikono, miguu na macho kama kutembea, kukimbia na kuogelea huzimakinisha hisia zako na kukuwezesha kujitambua na kuwatambua wengine zaidi baada ya shughuli zinazohusisha akili tu.

Pata usingizi wa kutosha. Enzi hizi zimejaa shughuli za kila namna, nyingi zikitukosesha usingizi. Mifumo ya chumi zetu inatushinikiza kulala kwa saa chache mno ili kufanikiwa maishani.

Inaelekea kwamba mwenyezi Mungu alikosea kutenga saa kumi na mbili za kupumzika, asilimia kubwa zaidi katika saa hizi ikitengewa usingizi. Tafiti zimedhihirisha kwamba watu wazima wanapaswa kulala kwa angalau saa saba unusu za kila usiku. Kisa na maana, kumbukumbu hukuzwa zaidi wakati wa usingizi mzito. Ili kuhakikisha hili kwa mujibu wa tafiti hizo ni muhimu kulala wakati ule ule na kwa kipindi maalum kila usiku, kujiepusha na viwambo kama vile televisheni na kompyuta takriban dakika thelathini kabla ya kulala na kupunguza matumizi ya kafeini.

Watengee rafiki zako muda. Waswahili tunaamini mtu ni watu. Hukamiliki bila rafiki. Wanasaikolojia pia wanakiri kwamba huu ni wenzo muhimu wa kukuza kumbukumbu. Kulingana na utafiti wa hivi majuzi kutoka Chuo cha Afya ya Umma cha Havard, watu wenye mahusiano mengi ya kijamii, wanaotagusana vilivyo na rafiki zao hupoteza kumbukumbu kwa kiasi kidogo zaidi.

Ila tu kwako mwanafunzi, hakikisha kwamba urafiki wako hauvuki mpaka ukawa uhusiano wa kingono. Aidha hakikisha unajiepusha na marafiki wenye mtazamo hasi Keanu watakuvuta nyuma hasa katika kipindi hike Cha maandalizi kwa mtihani.

Punguza msongo. Msongo ni mojawapo ya adui wakubwa wa akili. Una uwezo wa kuua seli za ubongo iwapo utaruhusiwa kuendelea kwa muda mrefu. Huharibu panapoundiwa kumbukumbu mpya, na kuvutia za zamani. Msongo unahusishwa na kupoteza kumbukumbu.

Ili kupunguza kiwango chako cha msongo: jiwekee malengo unayoweza kuyafikilia, kujipa breki katika shughuli zako za kila siku, kudhihiri hisia zako badala ya kuzificha na kuangazia shughuli moja kwa wakati mmoja.

Jizoeze kucheka. Kucheka ni sehemu muhimu ya uhai wetu. Kicheko huhusisha sehemu kubwa ya akili zetu na hivyo kukuza kumbukumbu. Miongoni mwa njia za kukuchekesha ni kuwaeleza wenzio hali iliyokukumba ulipodhihakiwa, kujiunga na watu wanaocheka na kushiriki uchangamfu wao. Kuwatazama watoto wakicheza na kujaribu kuwaiga katika baadhi ya michezo yao kunaweza pia kukuchekesha. Kwa jinsi hii waweza kuikuza kumbukumbu yako.

Yachunguze na kuyatatua matatizo ya afya kwa wakati. Ukigundua unapoteza kumbukumbu kwa kasi pasipo kufahamu chanzo, ni muhimu kuchunguzwa na tabibu au mwanasaikolojia ili kubaini chanzo na kupata matibabu.

Kudumu na tatizo hili bila kuchunguzwa ni kuhatarisha maisha kwani tunategemea kumbukumbu ili kufanikisha takriban shughuli zetu zote.

Nakutakia kila la heri unapojishughulisha kuikuza kumbukumbu yako.

You can share this post!

Majeraha kuwakosesha Coutinho na Fati wa Barcelona gozi la...

KINA CHA FIKIRA: Punguza mizigo mizito inayoweza kukuweka...