• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:55 AM
NDIVYO SIVYO: Aisee ndugu zetu wanahabari, tetesi si kisawe cha mgogoro!

NDIVYO SIVYO: Aisee ndugu zetu wanahabari, tetesi si kisawe cha mgogoro!

Na ENOCK NYARIKI

KATIKA taarifa mojawapo iliyopewa kipaumbele kwenye kituo kimoja cha runinga nchini, iliandikwa kichwa kifuatacho: ‘*Tetesi za LAPSSET’.

Maelezo ya kina ya taarifa yalihusu masuala ibuka ya mradi huo yakiwemo ardhi, fidia, umilikaji n.k.

Neno tetesi katika kichwa nilichokitaja lilikusudiwa kuchora taswira ya mtafaruku, malalamishi au kutoridhika kwa wakazi wa Lamu kuhusu mchakato mzima wa kuwafidia au kuhusu suala jingine liwalo linalohusu mradi wa LAPSSET.

Waama, neno tetesi si kisawe cha mzozo wala halipaswi kutumiwa kwa maana ya tukio au jambo lolote linaloibua mtafaruku, utata, kutoelewana au kutoridhika miongoni mwa watu. Neno hili linaweza kutumiwa tu wakati wa kuelezea taarifa au habari zisizothibitishwa kuwa kweli. Taarifa au habari hizi pia huelezewa kwa kutumia nomino uvumi, minong’ono, penyenye au fununu. Kuna neno utesi ambalo matamshi yake yanakaribiana na tetesi. Neno hili la pili linaweza kuwa chanzo cha mkanganyiko kama ule unaotokea katika kichwa cha taarifa nilichokitaja ambapo neno tetesi linatumiwa kimakosa kwa maana ya mzozo, mgogoro au mtafaruku unaohusu hali fulani.

Utesi ni nomino ambayo yamkini inatokana na kitenzi teta ambacho aghalabu huchukuliwa kwa maana ya kugombana au kutofautiana. Maana nyingine za kitenzi hicho jinsi zinavyojitokeza katika Kamusi Elezi ya Kiswahili ni kusema faraghani na kumsema mtu kwa mabaya wakati hayupo. Kwa hivyo, kutokana na kitenzi teta chenye maana ya kugombana au kutofautiana tunapata nomino utesi yenye maana ya hali ya kutoelewana miongoni mwa watu au ugomvi. Nomino nyingine inayoundwa kutokana na kitenzi hicho na ambayo inakumbatia maana ya pili jinsi inavyojitokeza katika kamusi tuliyoitaja ni mtesi. Neno mtesi lina maana mbili kuu. Kwanza, ni mtu mwenye tabia ya kuwasengenya watu wengine. Pili, ni mtu mwenye tabia ya kugombana na watu wengine kila mara.

Neno jingine ambalo linaweza kuchukuliwa kuwa kitate cha utesi, tetesi na mtesi ni mtetezi. Mtetezi ni nomino inayotokana na kitenzi tetea ambacho maana yake mojawapo ni kusaidia kutafuta haki ya mtu anayedhulumiwa au kunyanyaswa.

Alhasili, neno tetesi halipaswi kutumiwa kwa maana ya mzozo, mgogoro, mtafaruku au utata unaozunguka jambo au hali fulani. Wakati wowote vyombo vya habari vinapokiteua kichwa ili kukitumia kwenye taarifa fulani, ni muhimu kumakinikia uteuzi wa maneno.

Maneno hayapaswi kutumiwa tu kufidia ‘ombwe’ bali sharti yawasilishe maana iliyokusudiwa na inayojitokeza katika taarifa nzima au kwenye matini.

You can share this post!

LISHE: Ndizi na viazi

Mkopo wa Ighalo kambini mwa Man-United watamatika rasmi