• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 9:12 AM
Ndoto la straika huyo ni kuvalia chatu cha Messi

Ndoto la straika huyo ni kuvalia chatu cha Messi

Na PATRICK KILAVUKA

Analo ndoto moja katika ulingo wa soka yaani kuvaa chatu na jezi ya mwanasoka Lionel Messi wa PSG aliyetokea Barcelona.

Mfumaji Delvin Wayne Dzeko,16, anaonyesha dalili za kesho za kuwa mwanasoka chipukizi mithili ya Messi ambaye uchezaji wake umemvunia tija mbalimbali katika jukwaa la soka sawia na matarajio yake usoni. Anapokuwa uwanjani, mashabiki wanawachwa vinywa wazi kutokana na vitu anavyofanya ugani na kuiwezesha timu yake kutwaa ushindi.

Mwanadimba Wayne, mwanafunzi wa kidato cha pili Shule ya Upili ya Farasi Lane, Lower Kabete ana chenga za maudhi, pasi za hakika zinazozalisha magoli hali ambayo imeinua shule katika vipute mashinani na michezo ya shule.

Alianza kusakata kandanda akiwa kinda wa miaka mitano akiwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya Farasi Lane. Aidha, wakati huo, anasema alikuwa analelewa na timu ya mtaani ya Mwimuto Wailers ambako alianza kutolewa maruerue ya kisoka na ubutu kwenye kipaji chake cha kabambu akiwa katika timu ya wasiozidi miaka mitano.

Baada ya kuchongwa na timu ya mtaani ya Wailers, alihamia Diamond FC. Mchana nyavu huyo anadokeza kwamba hamna mwengine katika ya jamii yao aliye na kipaji cha soka. Wazazi wake Bw Amos Omindi na Bi Millicent Omondi ni wapenzi tu wa fani hii, japo wanamsapoti umbali amefika kisoka kwa ushauri na baadhi ya matakwa ya kikabumbu.

Starika Delvin Wayne Dzeko akiwa na kipa bora kutoka shule ya Loresho wakipiga picha ya na waliosimamia kagetoria ya shule za upili. Picha/PATRICK KILAVUKA

“Tuko kwetu wana watatu. Lakini mimi ndiye ninajitahidi kucheza boli kwa kujituma na nimeona mwanya wa upenyo wa talanta yangu,” asema mwanasoka huyo ambaye maono yake ni kwamba atahakikisha kwamba, chochote ambacho wazazi hakuweza kufanya kwa uwezo wa Mungu, atafaulu kufikisha ndoto hatimani!

Akiwa shule ya msingi, alishiriki katika michezo hadi kiwango cha Kanda ya Nairobi, iliyoandaliwa Shule ya Msingi ya Moi Forces, Nairobi kabla kuwakilisha Gatuzi la Nairobi kitaifa. Chini ya makocha Dan Ondim wa shule pamoja na anayemtambua kwa jina Fawa mshambuliaji huyo anapata msingi mwema wa ujuzi wa kumwezesha kustahamili dhoruba za kandanda.

Mbali na kuweka ruwaza yake hadharani kuwa ni moto wa kuotewa mbali. Shule yake imeshiriki katika kipute cha eneobunge la Westlands cha Westlands Youth Soccer almaarufu kama Tim Wanyonyi Super Cup makala ya nane na ameiwezesha kufika fainali kisha kutwaa taji la kitengo cha shule za sekondari kwa kuliza Shule ya Sekondari ya Loresho kwa kipigo cha 1-0.

Pamoja na kutawazwa mchezaji bora wa wavulana. Azma ya kuhusisha shule za upili katika patashika hilo ilikuwa kuchochea talanta na kuziangazia kwa timu zinazoshiriki ligi ya Shirikisho la Kandanda nchini kupata fursa ya kusaka talanta za mashinani.

Alifuma magoli mawili katika king’ang’anyiro hicho ingawa alivumisha mchezo wa timu. Anasema kupitia kipute hicho, amejifunza mawili matatu ya kujineemea katika kandanda. Hufanya mazoezi ya timu Jumatatu, Jumanne, Jumatano na Jumamosi iwapo hashiriki mechi yeyote ile.

Wakati mwingine anakumbatia masomo kama njia ya kujisawazisha kitalanta na masomo. Ujasiri wake, kuthibiti boli akicheza anasema unamsaidia kucheza soka fiti sana. Aidha, jitihadi za kujituma zimekuza ari ya kuimarisha soka yake na kuwa zao la ufanisi kwake kwa majaliwa ya Mwenyezi Mungu.

Anaamini kwa majaliwa anga ya kabumbu ikimfungulia milango ya ughaibuni, angependa kulivalia jezi la Barcelona. Ahimiza wachezaji kupiga shughuli ya boli kwa bidii ya mchwa tu na kufanya mambo kama timu ili, ufanisi uhakikishwa.

Mwanasoka chipukizi Delvin Wayne Dzeko wakati wa kupokea taji la mchezaji wa thamani (MVP) wa .Picha/PATRICK KILAVUKA

 

You can share this post!

Kocha aliyetumia miereka kunoa wanasoka wa Sagan Tosu...

Walibeba taji la Westlands Youth Soccer bila kushindwa

T L