• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
Nesi anayeuguza wagonjwa kwa nyimbo atuzwa

Nesi anayeuguza wagonjwa kwa nyimbo atuzwa

NA WINNIE ATIENO

MUUGUZI katika Hospitali Kuu ya Rufaa ya Pwani, amejizolea sifa kwa kujitolea kuimbia wagonjwa kama njia ya kuwapunguzia maumivu.

Ijumaa, Bi Rheater Shivikhwa alituzwa na Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe na Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, walipojulishwa kumhusu.

Walifahamishwa hayo alipowatumbuiza na wimbo wa uzalendo wa mwimbaji Eric Wainaina wa ‘Daima Mkenya’.

Alipoanza kuimba wagonjwa waliokuwa wamemiminika katika hospitali hiyo waliacha shughli zao ili kumtazama huku wale waliokuwa wamelazwa wakichungulia kwenye madirisha ya wodi zao wakimshangilia.

Bw Joho na Bw Kagwe walimpongeza na kumpa pesa. Papo hapo, Gavana aliamuru maafisa wake wakuu wa afya wamchangie pesa kama zawadi.

“Nilipoambiwa nitumbuize wageni mashuhuri wakati wa maadhimisho ya siku ya Saratani Ulimwenguni katika hafla ya kitaifa ambayo ilifanyika Mombasa Februari 4, nilishtuka. Hata hivyo, nilipiga moyo konde na nilipoanza kuimba kisha nikatazama nyuso za wagonjwa wa saratani, nilipata nguvu mpya,” alisema.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, muuguzi huyo mwenye umri wa miaka 26, alisema alianza kuwaimbia wagonjwa wake waliokuwa wamelazwa katika wodi ya wagonjwa waliotengwa wanaokabiliana na Covid-19 mapema mwaka wa 2020.

Lakini mkubwa wake aliposikia akiimba akamwambia arudie, ikawa ada. Akaanza kutumia kipawa chake kuwapunguzia maumivu na msongo wa mawazo wagonjwa wake na hata wenzake kazini.

“Huwa ninaimba kila mara isipokuwa ninapolala au nikila chakula. Hata nikiendelea na matibabu huwa najipata nikiimba. Siwezi kujizuia.

Kumbe wagonjwa wangu walikuwa wanafurahia, wakaanza kunisihi niendelee na mpaka leo huwa natumia sanaa hii kutibu wagonjwa,” alisema.

Lakini fahari yake kubwa ilikuwa ijumaa wakati Bw Kagwe na Bw Joho walipompongeza. Alimshukuru naibu mkuu wa hospitali hiyo Dkt Mercy Korir, kwa kumpa fursa hiyo.

“Wagonjwa wengi huwa na maumivu, lakini nyimbo huponesha moyo. Humpa mtu matumaini, nguvu na ari,” alisema.

Utotoni mwake, alipania kusomea masuala ya wanyama (Zoology and Animal Psychology) lakini babake akamsihi abadilishe nia na mnamo 2014, aliamua kusomea uuguzi katika Chuo Kikuu cha Kabarak.

Anasema alianza kuimba akiwa chekechea. Alipojiunga na shule ya msingi ya Consolata, na ile ya upili ya wasichana ya Kaaga huko Meru talanta yake ikapevuka. Baadaye akasomea shule ya sekondari ya Voi na mwishowe akamalizia Loreto Convent Valley Road iliyoko Nairobi.

Anasema babake amekuwa akiwahimiza kutumia muziki katika kila jambo. Bi Shivikhwa anayetambuliwa kwa jina Red. E alisema janga la corona lilimwathiri hasa wagonjwa wake walipoaga dunia. Ilimbidi aende kupokea nasaha.

“Inasikitisha kuona mgonjwa ambaye umemhudimia akiaga dunia. Hatua hii huwa inanifisha moyo mno,” aliongeza.

Alisema amepata uungwaji mkono kutoka kwa wakubwa wake na sasa Gavana na Waziri, jambo linalompa matumaini. Januari 26, alitoa wimbo wake wa kwanza. Anatumai kuendeleza uuguzi sambamaba na sanaa.

Anatumai ipo siku wauguzi na wasanii watapewa kipaumbele nchini kuliko ilivyo sasa.

  • Tags

You can share this post!

Siri ya kupunguza unene na uzani uliopitiliza

Maeneo yatakayoamua wazito kaunti za Pwani

T L