• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Njuri Ncheke wagawanyika kuhusu juhudi za kumtimua Kawira Mwangaza kwa mara ya pili

Njuri Ncheke wagawanyika kuhusu juhudi za kumtimua Kawira Mwangaza kwa mara ya pili

NA GITONGA MARETE

BUNGE la Kaunti ya Meru mnamo Jumatano, Oktoba 25, litajadili hoja ya kumtimua Gavana Kawira Mwangaza, kwa mara ya pili katika muda wa mwaka mmoja tangu alipoingia mamlakani.

Bunge la Kaunti hiyo linatarajiwa kuandaa vikao vya kushirikisha umma katika sehemu mbalimbali kaunti hiyo Jumatatu, Oktoba, 23, 2023.

Hata hivyo, huku vikao hivyo vikianza, mchakato unaotarajiwa kukumbwa na utata, hatua ya hivi majuzi ya Baraza la Wazee wa Njuri Ncheke ya kuunga mkono utimuaji huo imezua hisia kali na kuligawanya.

Mnamo Oktoba 14,2023, Baraza liliidhinisha mchakato wa kumng’atua Gavana katika hatua ambayo haikutarajiwa na iliyovutia mseto wa shutuma na sifa kwa usawa kwa kuwa wazee hao wa kitamaduni miaka yote wamekuwa wakiimuunga mkono gavana aliye mamlakani.

Katika hafla iliyofanyika kwenye madhabahu ya Nchiru, Tigania Magharibi na iliyoongozwa na Mwenyekiti Linus Kathera makatibu wawili, Josphat Murangiri (anayesimamia shughuli na Washington Muthamia (miradi), wazee waliwaruhusu madiwani wamng’oe Mwangaza mamlakani, wakisema ameshindwa kuunganisha jamii ya Ameru.

Ilishuhudiwa na Waziri wa Kilimo Mithika Linturi aliyetawazwa msemaji wa Meru, Waziri mwenzake wa Utalii Soipan Tuya, gavana wa zamani Kiraitu Murungi na wabunge wote tisa wa Meru.

“Baada ya jaribio la kwanza la kumtimua, tulijaribu kuzungumza naye lakini hakusikiza ushauri wetu na juhudi zetu za upatanisho zimegonga mwamba. Gavana amejawa na kiburi. Kama wazee, tunahisi imetosha kwa sababu huwezi ukaendesha kaunti ukiwa pekee yako,” alisema Bw Murangiri.

Bw Murungi alitangaza kuwa Naibu Gavana Isaac Mutuma atakuwa gavana wa nne wa Meru huku akimshutumu Bi Mwangaza kwa kushindwa “kuanzisha maendeleo ya maana” na kujishughulisha na mradi wake wa “Okolea” unaolenga wakazi maskini.

Kundi la wazee wa Njuri Ncheke kutoka Tigania Magharibi, Tigania Mashariki na Tigania ya Kati walisema walialikwa kwenye madhabahu ya Nchiru kwa hafla ya kupanda miti iliyogeuka ghafla mkutano wa kisiasa.

Wamepinga hatua ya uongozi wa Baraza kuegemea upande mmoja wakisema ni kinyume na kanuni za Njuri Ncheke.

Wazee hao vilevile wamekashifu hatua ya wenzao ya kuwabariki madiwani kabla ya hoja hiyo ya utimuaji iliyopangiwa kufanyika.

“Tumekataa kabisa maazimio yaliyofanywa kwenye madhabahu ya Nchiru. Taarifa ya Katibu Mkuu kwamba tunaunga mkono utimuaji wa Gavana Mwangaza haikutoka kwetu. Kikao ambapo maafikiano hayo yalifanyika hakikufaa kwa sababu kulikuwepo wanawake na watoto katika mkutano huo,” alisema Mzee kutoka Tigania Magharibi, Adriano Aruyaru.

Wachanganuzi sasa wamegawanyika kuhusu kitendo hicho cha wazee ambacho kimetikisa Baraza huku mtaalam wa utawala na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Multimedia, Profesa Gitile Naituli, akisema hatua hiyo haikufaa kwa sababu wazee wamefahamika kuunga mkono serikali inayotawala.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Wanaharakati, maafisa wasema baadhi ya wazee Malindi wana...

Gachagua sasa aomba mwafaka na mabroka wa kahawa ili...

T L