• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
NMS haijamaliza miradi ikisalia miezi 3 pekee

NMS haijamaliza miradi ikisalia miezi 3 pekee

Na COLLINS OMULO

MIEZI mitatu tu imesalia kabla ya muda wa uwepo wa Halmashauri ya Kusimamia Jiji (NMS) ambayo inasimamia majukumu manne makuu ya serikali ya Kaunti ya Nairobi kukamilika.

NMS ilichukua usukani mnamo Machi 2022 na imekuwa ikisimamia sekta za Afya, Uchukuzi, Miundomsingi na Maendeleo na Mipango ya Kaunti kwa muda wa miezi 24 iliyopita.

Na katika miezi yake sita kazini, NMS ambayo iliwekwa na serikali kuu ilitekeleza miradi ya maendeleo kwa kujenga maeneo yanayotumiwa na wanaotembea kwa miguu jijini.

Miradi hiyo ilijengwa kwenye barabara za Muindi Mbingu, Wabera na Kenya Avenue.

Pia NMS ilikarabati barabara jijini na mitaa mbalimbali huku pia ikikarabati na kuweka mabomba mapya ya majitaka, kujenga vituo vingine vya kiafya na kuweka taa kwenye barabara mbalimbali.

Ingawa hivyo, NMS haijazindua miradi mingine mipya katika mwaka wake wa pili kazini huku duru zikiarifu huenda mkataba wa uwepo wake ukaongezwa hadi Agosti, 2022.

Hata hivyo, bado hakuna notisi iliyochapishwa kuthibitisha nyongeza hiyo ya muda wa uwepo wa NMS.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba NMS inayoongozwa na Meja Mohamed Badi, imesalia na muda mchache kukamilisha miradi aliyoahidi raia.

Bw Badi alikuwa ameahidi kuwa kufikia 2022, NMS itakuwa imejenga hospitali 24, barabara zote kuu zingekuwa zimekarabatiwa kisha matatu na bodaboda zote kuondolewa katikati mwa jiji huku mabasi ya BRT na treni ikichukua nafasi hiyo.

“Nimekuwa mkazi wa Nairobi na nimeona matatizo ambayo yamekuwepo. Baada ya muda wa miaka miwili, nitakuwa nimetimiza mengi. Krismasi itakapowadia, Nairobi itakuwa kama Dubai huku barabara nyingi zikiwa zimewekwa lami na hospitali 24 mpya zikiwa zimejengwa,” akasema wakati wa kuadhimisha mwaka mmoja wa uwepo wa NMS.

Hata hivyo, licha ya kupokezwa Sh27.2 bilioni kugharimia miradi mbalimbali kwenye mwaka wa kifedha utakaokamilika June 30, 2022, miradi mingi imekwama huku mingine bado ikiwa haijaanzishwa.

Ujenzi wa daraja la City Square haujaanza, ukarabati wa nyuga za Uhuru Park na Central Park umesimamishwa na mahakama.

Magari ya umma, matatu na wahudumu wa bodaboda bado hawajaondolewa katikati mwa jiji.

You can share this post!

Atwoli, Oparanya wakagua Bukhungu matayarisho ya mkutano...

TAHARIRI: Tangazo kuhusu karo kuzifikia shule Jumatatu...

T L