• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
NWRL: Umul Qura yapania kucheza kila mechi kama fainali

NWRL: Umul Qura yapania kucheza kila mechi kama fainali

Na JOHN KIMWERE

LISILOKUWAPO moyoni, pia machoni halipo. Ni msemo unaoashiria kwamba hakuna linaloweza kutimia bila kufanyiwa kazi.

Pia unahimiza mhusika kuwa na mkakati mwafaka bila kuweka katika kaburi la sahau azimio analopania kufikia. Ingawa ndiyo mwanzo timu ya Umul Qura FC imeanza kupiga ngoma imetangaza kuwa katu haina lingine mbali imepania kukaza buti kuhakikisha inafuzu kupandishwa ngazi kushiriki kipute cha Ligi ya Taifa Daraja la Pili ndani ya miaka mitatu ijayo.

Umul Qura ni kati ya vikosi vinavyoshiriki mechi za Kundi B kuwania taji la Nairobi West Regional League (NWRL) muhula huu. Kikosi hicho kinatiwa makali na aliyekuwa mchezaji wa Harambee Stars, Issa Omondi akisaidiana na manaibu wake akiwamo Zakaria Didanke na Abdrashid Fabio na Abdihakim Xavi.

”Ingawa nyakati zingine tunapoteza mechi zetu naamini nina wachezaji wazuri wanaopania kujituma kwa udi na uvumba kwenye kampeni za muhula huu,” kocha Omondi aliyewahi kunoa Kayole Asubuhi alisema na kuongeza kuwa miaka ya sasa wazazi wengi wameruhusu wanao kuonyesha talanta zao.

Miaka sita ijayo

Anadokeza kuwa wamepania kupambana mwanzo mwisho kufukuzia tiketi ya kupandishwa daraja muhula ujao. Anashikilia kuwa sio rahisi kwa timu zinazoshiriki ligi za viwango vya chini kufanya vizuri lakini amepania kuhakikisha kuwa kikosi hiki kitafuzu kushiriki Ligi Kuu ya Betking Kenya Premier League (BKPL) ndani ya miaka sita ijayo.

Picha/JOHN KIMWERE

”Mimi ni mchezaji lakini nina imani tukijitolea, tushirikiane pia kujituma vizuri tutatizimiza azimio letu michezoni,” Abdisalam Hassan nahodha wa kikosi hicho alisema na kuongeza kuwa ingawa ndio mwanzo kushiriki migaragazano ya ngarambe hiyo wanalenga kutia bidii ili kuhepuka kushushwa ngazi.

Mara nne

Timu hii iliyomaliza ya pili kwenye mechi za Ligi ya Kaunti msimu uliyopita inajivunia kushinda kipute cha Greensport Africa mara mbili na kutawazwa wafalme wa shindano la Urban Arena mara nne. Makocha hao wanashikilia kwamba wachezaji hao wakitia bidii watafanya vizuri kwenye kampeni za muhula huu.

Naibu kocha, Zakaria anasema kuwa hakuna mteremko kwenye kampeni za ngarambe ya NWRL timu zote zinapambana kufa na kupona. ”Kundi letu linajumuisha wapinzani wakali kama KSG Ogopa FC, WYSA United, kemri FC na Melta Kabiria kati ya zingine,” akasema.

Umul Qura FC inajumuisha Boniface Indire, Vincent Ouma, Abdisalam Hassan(nahodha), Abdirahman Saeed, Abdirahman Hussein, Yunis Omar, Walid Abdiaziz, Ayanle Ali, Mohamed Dahir (naibu wa nahodha), Adnan Muktar, Yahya Hussein, Salah Ahmed, Mohamed Ali, Khalid Abdirizaq, Omar Hassan na Abdimalik Abdullahi.

Pia wapo Abdirahman Ahmed, Abdishakur Hassan, Mohamedkhathar Aftin, Zakariye Abdikarim, Abdirizak Abdullaahi, Adbiaziz Osman, Abdibasit Mahmoud, Abdikafi Abdirashid, Yussuf Hassanow, Mohamed Yussuf, Mohamed Ali, Ayub Abdullahi, Mohamed Abdikadir na Abdikafi Shariff.

Picha/JOHN KIMWERE
Timu ya Umul Qura FC inayoshiriki mechi za Ligi ya Nairobi West Regional League (NWRL).
  • Tags

You can share this post!

Msajili ajitenga na kashfa ya usajili vyamani

Kemri FC yaapa kupambana mwanzo mwisho