• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 7:55 AM
Nyamira sasa yajisimamia kusambaza huduma za maji

Nyamira sasa yajisimamia kusambaza huduma za maji

NA WYCLIFFE NYABERI

JUHUDI za Kaunti ya Nyamira kujitenga na majirani wao wa Kisii katika huduma za usambazaji wa maji safi ya kunywa, zimeshika kasi baada ya gatuzi hilo kusajili kampuni yao mpya, NYAWASCO.

Kwa muda mrefu, wakazi wa Nyamira wamekuwa wakisambaziwa maji na kampuni ya Gusii Water and Sanitation Company (GWASCO), yenye makazi yake Mjini Kisii.

Lakini viongozi wao wamekuwa wakidai GWASCO “inawabagua” na kwamba hawapokei huduma nzuri inavyohitajika.

Ili kuepuka “ubaguzi” huo, Gavana Amos Nyaribo wa Nyamira na viongozi wengine walianzisha mchakato wa kuiondoa Nyamira kutoka kwa usimamizi wa GWASCO.

Akitangaza kusajiliwa kwa kampuni hiyo mpya Jumanne, Novemba 21, 2023 diwani (MCA) wa Rigoma Nyambega Gisesa alisema wana kila sababu za kutabasamu kwani hivi karibuni, kampuni hiyo itaanza kutumikia wakazi wa Nyamira.

Bw Gisesa aidha alidokeza kuwa, kati ya kaunti 47 zilizoko nchini, ni kaunti nne tu ambazo hazikuwa na kampuni zao binafsi za maji safi na taka.

Kaunti hizo kulingana na Bw Gisesa ni Nyamira, Kisii, Transnzoia na Bungoma.

Hivyo, Bw Gisesa alisema uundwaji wa kampuni ya NYAWASCO ni jambo ambalo lilifaa kutekelezwa kitambo.

MCA huyo alieleza kuwa nia yao ya kujitenga na GWASCO haifai kusawiriwa kama yenye chuki bali ya kutoa huduma bora kwa raia ikizingatiwa kuwa maji ni hoja iliyogatuliwa.

“Nia ya kuanzisha kampuni yetu binafsi ya maji ni kuhakikisha wakazi wa Nyamira wanapewa huduma bora. Hii ni njia mojawapo kufanikisha ajenda za serikali ya gatuzi chini ya utawala wake Gavana Nyaribo,” Bw Gisesa alisema.

Septemba 2023, Bw Nyaribo aliidokezea kamati ya Seneti kuhusu Uwekezaji wa Umma wa Kaunti na Hazina Maalum (Senate County Public Investments and Special Funds Committee) kuhusu mipango hiyo.

Alipofika mbele ya kamati hiyo, Bw Nyaribo alisema GWASCO imekuwa ikikumbwa na changamoto nyingi zinazoathiri utendakazi wake.

“Nashukuru wanachama wa kamati hii kwa kukubaliana nasi kwamba Nyamira tunafaa kuwa na kampuni yetu binafsi ya maji baada ya kuwadondolea sababu zinazotukumba tukiwa chini ya GWASCO,” Gavana Nyaribo alisema alipokutana na maseneta.

Kamati hiyo inayoongozwa na Senata wa Vihiga Godfrey Osotsi, ilimhakikishia Gavana kuwa itaiandikia Bodi Inayodhibiti Huduma za Maji (Water Services Regulatory Board– WASREB) na serikali ya Kaunti ya Kisii ili mchakato wa kujitenga uanze mara moja.

GWASCO ina uwezo wa kusambaza maji zaidi ya kiubiki mita 15, 000 kwa siku.

Katika huduma zake, takribani watu 250, 483 wameunganishwa na maji ya mifereji.

Shughuli zake zilipigwa jeki baada ya serikali ya kitaifa, chini ya utawala wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kwa ushirikiano na Benki ya Ujerumani (KfW) kutoa msaada wa Sh1.5 billioni kuboresha miundomsingi yake.

 

  • Tags

You can share this post!

Mgeni aliye na mashtaka saba ya kunajisi watoto amjibu jaji...

Johana Chacha: Mwanahabari wa zamani akiri kuwa mateka wa...

T L