• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
Nyayo House kuna maradhi ya ufisadi, akiri Kindiki

Nyayo House kuna maradhi ya ufisadi, akiri Kindiki

NA CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki mnamo Alhamisi alikiri kuwa ufisadi umekita katika kitengo cha utoaji pasipoti katika jumba la Nyayo jijini Nairobi, na kuahidi kutokomeza uovu huo.

Prof Kindiki alitaja kitengo hicho kama eneo la uhalifu na kuapa kupambana na magenge ya watu au maafisa ambao huhujumu haki ya Wakenya ya kupata stakabadhi hizo muhimu.

“Uchunguzi wetu umebaini kuwa kuna maafisa katika kituo cha utoaji pasipoti katika Nyayo House ambao huitisha hongo kutoka kwa Wakenya hata kwa huduma ambazo wanapaswa kupata bila malipo,” akasema alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Utangamano wa Kikanda chini ya uongozi wa Naibu Mwenyekiti Farah Salah Yakub (Mbunge wa Fafi, UDA).

“Nitahakikisha kuwa wafisadi wote wameondolewa Nyayo House. Tutafunga jumba la Nyayo House na kulitaja kama eneo la uhalifu,” Prof Kindiki akaeleza.

Waziri alisema ingawa mikakati imewekwa kuhakikisha kuwa jumla ya pasipoti 5,000 zinatengenezwa kwa siku moja, wakati huu jumla ya maombi 58,000 ya pasipoti hayajashughulikiwa.

“Bila shaka kucheleweshwa huku kwa utengenezaji wa pasipoti kunasababishwa na ufisadi. Huu ndio uovu ambao tunataka kupambana nao ili muda wa kupatikana kwa pasipoti upunguzwe hadi siku saba,” Prof Kindiki akasema.

Waziri aliwaambia wabunge hao kuwa siku moja yeye mwenyewe amewahi kufanya ziara ya ghafla katika jumba la Nyayo majira ya asubuhi na kukumbana na foleni ndefu ya Wakenya wanaotaka kutuma maombi ya pasipoti.

“Hii ndio maana niliketi na maafisa husika na kuwaonya kwamba hali kama hiyo hairuhusiwi kuendelea kushuhudiwa kwani Wakenya wanafaa kuhudumiwa kwa haraka iwezekanavyo,” akaeleza.

Waziri alisema baada ya mashine ya kuchapisha pasipoti kufanyiwa ukarabati, muda wa kutengenezwa kwa stakabadhi hizo utapunguzwa hadi siku saba.

  • Tags

You can share this post!

Wanaokataa kulipa mkopo wa Hasla kujuta

Vihiga Queens kuanza dhidi ya Ulinzi Starlets msimu mpya wa...

T L