• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 2:08 PM
Nzoia Sugar FC wampa kazi kocha Ibrahim Shikanda

Nzoia Sugar FC wampa kazi kocha Ibrahim Shikanda

Na CHRIS ADUNGO

NZOIA Sugar wamemteua kocha wa zamani wa Nairobi Stima, Ibrahim Shikanda, kudhibiti mikoba yao.

Mkufunzi huyo ameaminiwa kuwa mrithi wa Sylvester Mulukurwa ambaye kwa sasa atakuwa kocha msaidizi. John Muraya atasalia kuwa mkufunzi wa makipa.

Nzoia Sugar hawajakuwa na mkufunzi tangu Machi mwaka huu baada ya Collins ‘Korea’ Omondi kutimuliwa kwa sababu ya matokeo duni. Chini ya Korea, Nzoia Sugar waliambulia nafasi ya 15 kwa alama 13 kutokana na mechi 22 kwenye msimamo wa jedwali la vikosi 18 vya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) mnamo 2019-20.

Shikanda amewahi pia kuwa kocha msaidizi wa Bandari FC. Akiwa huko, alishirikiana na Nassor Mwakoba kumsaidia Bernard Mwalala aliyetimuliwa na kikosi hicho cha Pwani ya Kenya mwanzoni mwa mwaka huu.

Hadi alipoingia Bandari FC ambao walimtema mnamo Juni mwaka huu, Shikanda alikuwa pia amehudumu kama kocha msaidizi kambini mwa Azam FC ya Tanzania kati ya 2008 na 2013.

Chini ya Mulukurwa ambaye amekuwa mshikilizi wa mikoba ya Nzoia tangu Korea aondolewe, kikosi hicho kilianza vibaya kampeni za Ligi Kuu ya FKFPL msimu huu kwa kichapo cha 2-o kutoka kwa Nairobi City Stars mnamo Novemba 29 uwanjani Nyayo, Nairobi.

Ni matarajio ya Evance Kadenge ambaye ni mwenyekiti wa Nzoia Sugar kwamba wanasukari hao sasa watajinyanyua chini ya kocha mpya ambaye kibarua chake cha kwanza kitakuwa dhidi ya Kariobangi Sharks mnamo Jumamosi uwanjani Sudi, Bungoma.

Sharks watajibwaga ugani kwa mchuano huo wakipania kuendeleza ubabe uliowashuhudia wakipepeta Wazito FC 4-0 wikendi iliyopita uwanjani MISC Kasarani.

Kwa mujibu Kadenge, jopo lililosimamia mahojiano ya baadhi ya wakufunzi waliotuma maombi ya kazi kambini mwa Nzoia Sugar lilitoa majina ya wawaniaji watatu wa mwisho kwa Bodi ya Usimamizi.

Mbali na Shikanda, wengine ni kocha wa zamani wa Harambee Stars, James Nandwa na mkufunzi wa zamani wa SoNy Sugar, Leonard Odipo. Nandwa amewahi pia kuwa mkufunzi mkuu wa Thika United. Watatu hao waliunga orodha ya mwisho baada ya mchujo wa kwanza ambao ulivutia jumla ya wakufunzi 24 wakiwemo kocha wa zamani wa Shabana FC, Gilbert Selebwa, aliyekuwa kocha msaidizi wa KCB Ezekiel Akwana, John Kamau, Francis Xavier, George Maina, John Nams na Yusuf Chipo.

Kamau ameteuliwa kuwa msaidizi wa aliyekuwa kocha wa Harambee Stars, Francis Kimanzi, katika kikosi cha Wazito FC kilichomtimua majuzi Fred Ambani na benchi yake nzima ya kiufundi iliyomjumuisha pia kocha Salim Babu ambaye sasa ameajiriwa na Kisumu All Stars.

Nzoia Sugar ambao walipokea basi jipya lenye viti 51 na Sh2 milioni kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta hivi majuzi, kilijisuka upya kwa kusajili wanasoka 12 baada ya kuagana na wachezaji tisa muhula huu.

  • Tags

You can share this post!

Mswada wa kuboresha kilimo cha majanichai washabikiwa na...

Kocha Patrick Vieira afutwa kazi baada ya matokeo duni ya...