• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:45 AM
CECIL ODONGO: Oburu apewe useneta lakini si kwa sababu ya jina la Odinga

CECIL ODONGO: Oburu apewe useneta lakini si kwa sababu ya jina la Odinga

Na CECIL ODONGO

HUKU kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022 zikiendelea kushika kasi, Kinara wa ODM Raila Odinga alijipata kona mbaya akikashifiwa mitandaoni kwa kumuidhinisha kakake, Dkt Oburu Oginga kuchaguliwa seneta wa Siaya.

Bw Odinga alikaangwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya kutoa tangazo hilo wakati wa misa ya kuadhimisha Krismasi katika kanisa la AIC, Nyamira, Bondo.

Waziri huyo mkuu wa zamani alisema ukongwe wa kakake haufai kutumiwa kumnyima nafasi ya uongozi ila wapigakura wazingatie uzoefu na hekima- sifa ambazo atatumia kutetea wakazi wa Siaya katika Bunge la Seneti.

Aidha, alisisitiza kuwa kiongozi wa sampuli ya Dkt Oginga hafai kuwabembeleza wapigakura wamchague wala yeye mwenyewe hafai kurejea Siaya kuwarai wapigakura wachague Dkt Oginga, 79 kama Seneta na James Orengo, 70, kama gavana.

Kauli ya Bw Odinga inaafiki na Wakenya wanafaa wakome kumkashifu kutokana na hatua ya kumuidhinisha nduguye kumenyania kiti cha Useneta wa Siaya 2022. Dkt Oginga hafai kunyimwa haki yake ya kikatiba kutokana na uhusiano wake na ‘baba’ ambaye analenga urais kwa mara ya tano.

Ni wapigakura wanafaa wamkumbali au wamkatae debeni badala suala hili kutumika hata na wapinzani wa Bw Odinga kwenye siasa za kitaifa kumharibia nafasi ya kuingia ikulu.

Kwa kurejelea historia, Dkt Oginga aliingia bungeni kwenye uchaguzi mdogo wa 1994 ili kurithi kiti cha Bondo baada ya kifo cha babake Jaramogi Oginga Odinga aliyekuwa makamu wa Rais wa kwanza Kenya.

Alihudumu kama mbunge wa Bondo hadi 1994 na kutoka 2002-2013, matokeo ya tafiti mbalimbali za matumizi ya fedha zilizotengewa Hazina ya Kitaifa ya Ustawi wa Maeneobunge Nchini (CDF) iliorodhesha eneobunge hilo kati ya yale yaliyokuwa yakitumia vyema pesa zake kwa miradi ya maendeleo.

Aidha, mwanasiasa huyo pia alihudumu kama Waziri Msaidizi wa Fedha kwenye serikali ya ‘nusu mkate’ kutoka 2008-2013.

Hata hivyo, jaribio lake la kuwania kiti cha Useneta 2013 lilikosa kutimia alipoachia Bw Orengo nafasi hiyo na kupigania kiti cha Ugavana dhidi ya William Oduol kwenye mchujo wa ODM uliozingirwa na utata huku wawili hao wakipigwa kumbo na chama kisha Cornel Rasanga kupokezwa tiketi hiyo.

Kwa hivyo, Bw Odinga hadanganyi kuwa kake ana uzoefu kwenye siasa na pia wakati wake kama mbunge, Bondo ilipiga hatua kubwa kimaendeleo.

Ingawa kigezo cha umri si hoja sana mradi kiongozi ni mchapakazi, kile ambacho huenda kinawahofisha kizazi cha sasa ni umri mkubwa wa Bw Orengo kama Gavana na Dkt Oginga kama seneta.

  • Tags

You can share this post!

Mwimbaji bingwa ‘General Defao’ 62, aaga dunia

Hofu wazee wakipoteza pesa katika kamari

T L